TPDC YATOA MILIONI 56 KUJENGA VYOO MASHULENI MKOANI LINDI

Choo kipya cha Hingawali kilichojengwa kwa udhaminii wa TPDC

Katika hatua za kuhakikisha sekta ya elimu nchini inaimarika, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 56 ili kutatua kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa vyoo unaoukabili Shule za Msingi Mkoani Lindi.

Akitoa ufafanuzi juu ya fedha hizo, Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi.Marie Msellemu alisema kuwa Shule tano za Msingi mkoani Lindi zimepata msaada wa jumla za shilingi milioni 56 kwajili ya ujenzi wa vyoo baada ya kugundua tatizo la vyoo mashuleni mkoani humo huku akitaja shule hizo kuwa ni shule ya Msingi Madangwa, Hingawali, Ng’apa na Mkupama ambazo kila shule ilipewa kiasi cha shilingi Milioni 10 kwajili ya kuboresha vyoo katika shule hizo, huku Shule ya Msingi Kivinje wilayani Kilwa ikipewa kiasi cha shillingi million 16 kwa ajili ya ujenzi wa choo.

Akikabidhi rasmi vyoo hivyo kwa Mamlaka mbalimbali za shule hizo, Januari, 2019, Bi. Msellemu alisema kuwa TPDC inayo Sera Mfuko wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambao unatumika kurudisha kwa jamii kwa maeneo ambayo kuna uwekezaji wa miradi ya TPDC.

“TPDC inao mfuko wa CSR unaotumika kurudisha kwa jamii katika maeneo ambayo miradi ya TPDC inatekelezwa katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dar es salaam, na katika Mkoa wa Lindi tumeweza kuchangia kiasi cha milioni 56, ambapo milioni 16 zilikwenda Kilwa Kivinje kwa masuala ya kujenga vyoo, Madangwa, Hingawali, Mkupama na Ng’apa pia walipewa milioni kumi kila shule kwajili pia ya ujenzi wa vyoo na jumla kukamilika kuwa milioni 56.”

Kwa kupitia mfuko huu wa kurudisha kwa jamii, TPDC imejikita zaidi katika kuboresha huduma za kijamii kwa maana ya elimu, afya, maji na utawala bora. Msukumo wa kuboresha hali ya vyoo katika shule hizi unalenga kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na afya njema na kuweza kusoma katika mazingira bora.

Aliendelea, “Tunategemea watoto wetu kuwa na utamaduni wa kutumia vyoo lakini pia tunaamini tunawajenga katika mazingira ya kujali afya zao jambo ambalo litawawezesha kusoma kwa utulivu lakini vile vile kuwajengea tabia ya kuendeleza usafi hadi majumbani kwao kwa kusisitiza matumizi ya vyoo bora” alisema Bi. Msellemu.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ng’apa, Mwl. Hamis Abdallah, alitoa shukurani kwa TPDC kwa kutoa milioni 10 na kufadhili ujenzi wa choo chenye matundu sita kwajili ya Wanafunzi na matundu mawili kwajili ya Walimu.

“Kwa kipekee, ninaishukuru TPDC kwa kutatua tatizo la vyoo shuleni kwetu kwani wanafunzi hawakua na vyoo bora vya kutumia lakini pia kabla ya hapo, walimu pia walikua hawana vyoo hivyo ililazimika kwenda kutumia vyoo vya nyumba za walimu wanaoishi karibu na shule, lakini kupitia msaada huu wa TPDC, tumeweza kutatua changamoto hii ambayo hatukuweza kupata suluhisho kwa haraka.”

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Shule ya Msingi Madangwa alishukuru TPDC kwa mchango na ufadhili wa vyoo vya matundu nane kilichotatua changamoto ya vyoo shuleni hapo.

“Kutokana na upungufu wa matundu ya vyoo, TPDC waliona ipo sababu ya kutupatia msaada wa ujenzi wa vyoo vya wasichana matundu 8 ambavyo hadi sasa vimeshakamilika na kuanza kutumika tangu 2017” alisema Mwl. Juma Hamisi ambae ni Mkuu wa Shule ya Msingi Madangwa.

Aidha, kwa upande mwingine, mwanafunzi wa shule ya Madangwa Habib Issa akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, aliishukuru TPDC na kuelezea faida walizopata kwa kuboreshewa mazingira ya vyoo shuleni kwao.

“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Shirika la TPDC kwasababu wametuendeleza katika maendeleo ya shule yetu hususani kwa kutujengea choo kwajili ya wavulana na wasichana ambapo sasa vyoo vina hali nzuri tofauti na hapo awali ambapo kulikua na changamoto.”

Akiongea katika mkutano mfupi uliofanyika shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hingawali Mwl.Osbert Mzesse alikiri kuwa uongozi wa shule ulipokea fedha za ujenzi wa vyoo hatua ambayo imeshakamilika na kuanza kutumiwa na wanafunzi. Aidha aliipongeza TPDC kwa hatua ya kuwafadhili shule yao na kuwajengea choo chenye ubora.

“Tunaishukuru sana TPDC kwa ufadhili huu kwani umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la vyoo shuleni hapa” alisema Mwl. Mzesse.

Taarifa ya Mwalimu Mkuu ilieleza kabla ya mradi mwaka 2016, Shule ilikuwa na matundu 8 tu yaliyochakaa na idadi ya wanafunzi ilikua 483 hivyo kuwa na changamoto kubwa ya utumiaji wa vyoo, lakini baada ya mradi huu mwaka 2019 shule ina matundu 16 yanayoweza kuhimili wingi wa wanafunzi kwa sasa shuleni hapo.

Choo kilichokua kinatumika awali Shule ya msingi Hingawali

Choo kilichokua kinatumika awali Shule ya msingi Hingawali

Choo kipya cha Hingawali kilichojengwa kwa udhaminii wa                                                                        TPDC

Choo kipya cha Hingawali kilichojengwa kwa udhaminii wa  TPDC

Katika Wilaya ya Kilwa, Shule ya Msingi Kivinje ni moja ya shule zilizopewa fedha na TPDC kwajili ya ujenzi wa vyoo. Shule hiyo ilipewa kiasi cha shillingi milioni 16 na ujenzi umeshakamilika shuleni hapo ambapo wamejenga vyoo vyenye matundu 20 ikiwa 10 kwa ajili ya Wasichana na 10 kwa ajili ya Wavulana.

Akielezea kuhusu vyoo hivyo, Mkuu wa Shule ya Msingi Kivinje Mwl.Abbas Ngabuma alisema kuwa vyoo hivyo sasa viko katika hatua ya mwisho kukamilika na baada ya muda mfupi wanafunzi wataanza kuvitumia. Aidha, alitoa shukurani kwa TPDC kwa kuona umuhimu wa kuboresha mazingira ya vyoo shuleni kwao

Choo cha awali cha S/M Kivinje

Choo cha awali cha S/M Kivinje

Choo kipya cha S/M Kivinje kilichojengwa kwa                                                             Ufadhili wa TPDC

Choo kipya cha S/M Kivinje kilichojengwa kwa  Ufadhili wa TPDC

Katika kuhitimisha zoezi la kukabidhi rasmi vyoo hivyo, Bi. Msellemu alishukuru uongozi wa shule hizo kwa kutumia fedha hizo kadri ya matumizi yaliyo kusudiwa na ambapo  Shirika limeridhishwa na ubora, na matumizi sahihi yaliyotumika katika kufanikisha ujenzi huo wa vyoo na pia kuahidi kuwa TPDC ipo kwa ajili ya maendeleo ya jamii ambayo ndiyo maendeleo ya Taifa.

 

 

 


Comments