DC MWAIPAYA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UTAFUTAJI MAFUTA NA GESI ASILIA KITALU CHA LINDI-MTWARA

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya, ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika Kitalu cha Lindi-Mtwara, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Mhe. DC Mwaipaya alieleza kuridhishwa huko baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, akisisitiza namna TPDC inavyotumia teknolojia ya kisasa ya mitetemo (3D Seismic) katika shughuli zake.
"Uwekezaji huu ni muhimu na unatafsiri kwa vitendo jitihada za Serikali za kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia nchini, ambayo imekuwa na mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa Taifa letu," alisisitiza Mhe. Mwaipaya.
Akitoa maelezo ya kitaalamu hapo awali, Meneja wa Mradi kutoka TPDC, Dkt. Shaidu Nuru, alifafanua kuwa lengo kuu la mradi huu ni kupata taarifa za hali ya miamba iliyopo chini ya ardhi, ikiwemo muundo wa miamba na viashiria vya uwezekano wa uwepo wa hifadhi ya mafuta au gesi asilia.
Dkt. Nuru alieleza kuwa “ukusanyaji wa taarifa za mitetemo unafanywa kwa mfumo wa 3D (Three-Dimensional) na unajumuisha takribani kilomita za mraba 736.”
Mradi huu wa kimkakati unatekelezwa katika jumla ya vijiji 48 vilivyopo ndani ya Halmashauri mbili tofauti: Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi, ambapo kati ya hivyo, vijiji 40 vipo halmashauri ya Mtwara na vijiji 8 vipo Halmashauri ya Mtama.
Aidha, Mradi umetoa na unaendelea kutoa ajira za ujuzi maalumu na zile za vibarua kwa jamii zinazozunguka mradi, ambapo hadi kufikia tarehe 05/10/2025 ajira zaidi ya 1,212 zimetolewa kwa jamii hizo, kati ya hizo, ajira 404 ni kupitia TPDC.




