EACOP NI MRADI BORA ZAIDI DUNIANI KWA KUJALI UTU NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA –BALOZI OMBENI SEFUE

Haya yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhe. Balozi Ombeni Sefue alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Alexander Mhando mjini Korogwe mkoani Tanga
Akizungumza katika kikao hicho Balozi Sefue amesema kuwa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga Tanzania (EACOP) ndio mradi bora duniani kwa sasa ambao umezingatia kwa kiasi kikubwa haki na stahiki za waliopitiwa na mradi, usalama na utunzaji wa mazingira, ajira na uboreshaji wa maisha ya watanzania.
“Haikuwa rahisi kama nchi kuupata huu mradi kwa sababu chaguzi za njia ya kupitisha bomba zilikua nyingi na hivyo mafanikio ya kwanza kama nchi ni kufanikiwa kuupata huu mradi lakini kwa sasa kama nchi tumeendelea kunufaika zaidi kama vile kuongeza pato la Taifa pamoja na fidia nzuri walizolipwa watanzania waliopitiwa na mradi na kandarasi mbalimbali kwa makampuni ya kizalendo,” ameeleza Balozi Sefue.
Aidha Sefue amesisitiza kwa kipindi kilichobaki cha kukamilisha ujenzi tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa wakati.
Katika Wilaya ya Korogwe mradi unahusisha Shughuli za utandazaji wa bomba kwa urefu wa kilomita 6.68 ambapo jumla ya wananchi 26 pekee ndio waliopitiwa na kulipwa jumla ya shillingi milioni 174.