>
emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
ega Logo
Habari
svg-tree

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius John Ndenjembi amefanya ziara fupi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) tarehe 24/11/2025 na kukutana na Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Shirika hilo kwa madhumuni ya kufahamiana na kuweka misingi imara katika utekelezaji wa majukumu ya sekta ya mafuta na gesi nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Ndenjembi aliipongeza TPDC kwa hatua mbalimbali za kimkakati ilizochukua katika usimamizi wa rasilimali ya gesi asilia na mafuta, na kusisitiza umuhimu wa kasi, uwazi na ubunifu katika kuendeleza miradi ya kimkakati yenye manufaa kwa Taifa.

“Tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. Nataka kuona TPDC inasimama imara kama nguzo ya Taifa katika usimamizi wa nishati, inayochochea uchumi, ajira na maendeleo ya kijamii,” alisema Ndenjembi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue aliihakikishia Serikali kuwa Bodi hiyo itaendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa Shirika, kuhakikisha nidhamu ya kiutawala, ufanisi wa rasilimali, na utekelezaji wa miradi mikubwa kama vile usambazaji wa gesi majumbani, viwandani, pamoja na maandalizi ya miradi ya LNG.

“Bodi imejipanga kuhakikisha TPDC inafanya kazi kwa viwango vya juu, kwa uadilifu na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Tutaendelea kuboresha mifumo, kusimamia mikakati na kuimarisha utendaji wa Menejimenti ili kufikia matarajio ya Serikali na wananchi,” alisema Balozi Sefue.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Ndugu Mussa Makame, alitumia nafasi hiyo kutoa taarifa ya utendaji wa Shirika, mafanikio ya hivi karibuni na malengo ya muda mfupi na mrefu, ikiwemo kuimarisha usambazaji wa gesi asilia nchini, kuongeza ushiriki wa Watanzania katika miradi ya mafuta na gesi, na kukuza ubunifu unaolenga kupunguza gharama za uzalishaji na matumizi ya nishati.

“TPDC imejipanga kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya gesi asilia kwa matumizi ya majumbani, viwandani, magari na katika uzalishaji umeme. Tutaendelea kushirikiana na Serikali, wadau na wawekezaji kuhakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha Watanzania wote,” alisema Makame.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji aliahidi kwamba katika kipindi cha siku miamoja za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, TPDC itakuwa imeshapiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuweza kuleta tija katika uchumi wa taifa.

Ziara hiyo imehitimishwa kwa Mhe. Ndenjembi kupongeza juhudi za Bodi na Menejimenti na kutoa rai ya kufanya kazi kwa mshikamano, weledi na uwajibikaji, kwa maslahi ya Taifa.

Mpangilio