>
emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
ega Logo
Habari
svg-tree

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) baada ya kutembelea na kukagua utekelezaji wake katika eneo la Chongoleani, mkoani Tanga, akieleza kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati kwa Tanzania, Uganda na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imewekeza shilingi bilioni 973 katika mradi huo unaohusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilometa 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 87, huku ukitarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 ifikapo mwishoni mwa Agosti 2026. Ameongeza kuwa matarajio ni kwamba meli ya kwanza itapakia mafuta ghafi katika Kituo cha Chongoleani mwezi Januari 2027, hatua itakayoashiria kuanza rasmi kwa usafirishaji wa mafuta kupitia bomba hilo.

“Mwaka huu ni hatua muhimu katika historia ya sekta ya nishati kwani mradi huu ni wa kimkakati kwa Tanzania, Uganda na Afrika Mashariki kutokana na mchango wake katika kukuza uchumi, kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira kwa wananchi,” alisema Waziri Ndejembi.

Aidha, aliwataka Watanzania kuendelea kutumia fursa zinazotokana na mradi huo, akibainisha kuwa zaidi ya Watanzania 3,000 tayari wamepata ajira zinazohitaji ujuzi mbalimbali, huku maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja zikiendelea kuzalishwa kupitia shughuli za utekelezaji wa mradi.

Mhe. Ndejembi pia alisema TPDC imewapeleka vijana 100 katika Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba mkoani Mtwara kwa mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea uwezo wa kushiriki katika uendeshaji wa mradi huo. Vilevile, zaidi ya vijana 400 kutoka Chongoleani wamepata ajira kupitia utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Juni 30, 2026, Waziri ataendelea na ziara yake katika Wilaya ya Handeni, ambapo atakagua eneo la Pressure Reduction Station ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa maendeleo ya mradi huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Buriani, amesema Mkoa wa Tanga unaendelea kunufaika na matokeo chanya ya mradi huo kupitia ongezeko la ajira, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi zinazoboresha maisha ya wananchi.

Dkt. Buriani alimpongeza Mhe. Ndejembi kwa usimamizi madhubuti wa sekta ya nishati na kueleza kuwa maendeleo ya mradi yanaendelea vizuri, huku ujenzi wa eneo la matenki ya kuhifadhi mafuta ukiwa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayochochea maendeleo ya Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.

Mpangilio