>
emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
ega Logo
Habari
svg-tree

Mtwara, Februari 27, 2026

Mradi wa Gesi Asilia-Ntorya ukamilike Septemba 2026

Waziri wa Nishati, Deogratius John Ndejembi, ametoa maelekezo mahsusi kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha Mradi wa Maendeleo ya Gesi wa Ntorya unatekelezwa kwa kuzingatia nidhamu ya muda na viwango vya kitaalam, ili visima vya gesi vianze rasmi uzalishaji ifikapo Septemba 2026 kama ilivyopangwa.

Waziri Ndejembi alitoa maelekezo hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Ntorya kwenda Madimba, uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara. Alisisitiza kuwa Serikali inatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja ya uwekezaji huo wa kimkakati bila visingizio vya ucheleweshaji.

“Serikali inataka kuona utekelezaji wenye tija na unaoendana na ratiba. Septemba 2026 siyo pendekezo bali ni lengo mahsusi la kuanza uzalishaji,” amesisitiza Waziri Ndejembi.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Ndejembi, Mradi wa Gesi wa Ntorya sasa umeingia katika hatua ya utekelezaji rasmi kufuatia kuanza kwa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwenda Madimba. Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi muhimu ya kuwezesha uchakataji na usafirishaji wa gesi kwa matumizi ya ndani ya nchi.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza upatikanaji wa gesi asilia nchini, kuimarisha usalama wa nishati, na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za Serikali za kuongeza uzalishaji wa umeme kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Pamoja na suala la kukamilisha mradi kwa wakati, Waziri Ndejembi amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya TPDC, wakandarasi, na viongozi wa maeneo husika ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi unazingatia maslahi ya wananchi, hususan kupitia miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

“Miradi ya CSR inapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya mradi mkuu, ili jamii zinazozunguka eneo la mradi zinufaike moja kwa moja na uwekezaji huo,” amebainisha Waziri wa Nishati.

Mradi wa Gesi wa Ntorya ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuendeleza rasilimali za gesi asilia kwa manufaa ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme, kukuza viwanda, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kupitia usimamizi madhubuti na utekelezaji kwa kuzingatia ratiba, mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa sekta ya nishati na ustawi wa wananchi.

 

Mpangilio