Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Aitaka TPDC Kuimarisha Uwekezaji katika Gesi Asilia

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, ameielekeza Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuimarisha uwekezaji katika sekta ya gesi asilia kwa kuongeza vitalu vipya vya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi nchini.
Dkt. Mataragio alitoa maelekezo hayo alipofanya ziara katika ofisi za TPDC jijini Dar es Salaam na kufanya kikao kazi na Menejimenti ya Shirika hilo kilicholenga kujadili maendeleo, changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi nchini.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio aliambatana na Kamishna wa Petroli Goodluck Shirima pamoja na Kamishna Msaidizi wa Mkondo wa Juu wa Petroli, Raphael Antelimi, kutoka Wizara ya Nishati.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mataragio alisema ziara zake katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinalenga kupata uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa majukumu, changamoto na fursa zilizopo ili kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya nishati nchini.
“Tunafanya ziara hizi ili kusikiliza changamoto zilizopo, kutambua fursa na kuweka mikakati ya kuimarisha sekta ya nishati ambayo ni mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisema Dkt. Mataragio.
Alisisitiza kuwa TPDC ina jukumu muhimu katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi nchini, hivyo ni lazima iendelee kupanua maeneo ya uwekezaji ili kuongeza ushindani na kuvutia wawekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa rasilimali hizo.
Aidha, aliagiza Menejimenti ya TPDC kusimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi ya gesi asilia, akibainisha kuwa miradi hiyo ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika hususan katika uzalishaji wa umeme na kukuza uchumi wa viwanda.
Alieleza kuwa gesi asilia ni rasilimali muhimu inayochangia kupunguza utegemezi wa vyanzo vingine vya nishati na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati nchini, hivyo utekelezaji wa miradi yake unapaswa kupewa kipaumbele cha juu.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi ya gesi asilia inatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuongeza matumizi ya nishati hiyo katika sekta mbalimbali za uchumi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Petroli Goodluck Shirima alisema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia ili kuongeza matumizi yake katika sekta mbalimbali ikiwemo majumbani, viwandani na katika uzalishaji wa umeme.
“Mahitaji ya gesi asilia yanaendelea kuongezeka, hivyo ni muhimu TPDC ikaweka kipaumbele katika miradi ya usambazaji wa gesi ili wananchi na sekta ya viwanda waweze kunufaika zaidi na rasilimali hii,” alisema Shirima.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kutenga na kuandaa maeneo kwa ajili ya ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya usambazaji wa gesi asilia, akieleza kuwa miradi hiyo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuongeza matumizi ya gesi katika uzalishaji wa umeme, majumbani na viwandani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, alishukuru ujio wa Katibu Mkuu na ujumbe wake na kuahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwa maslahi ya Shirika na taifa kwa ujumla.




