>
emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
ega Logo
Habari
svg-tree

Mradi wa Utafutaji Mafuta wa Eyasi Wembere unaendelea kuwa kielelezo cha ubora, ufanisi na uwezo wa kitaalamu ambao Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania limeujenga katika sekta ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC, Balozi Ombeni Sefue, alisema tangu kuanza kwa shughuli za utafiti mwaka 2015 hadi sasa, TPDC imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 47 zinazotokana na fedha za ndani za Shirika kutekeleza mradi huo.

Alisema uamuzi wa kuwekeza katika Bonde la Eyasi Wembere umetokana na tafiti za kijiolojia zinazoonesha kuwa eneo hilo linafanana na maeneo ya Lake Albert nchini Uganda pamoja na Turkana nchini Kenya ambako tayari mafuta yamegunduliwa ndani ya Ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.

Aidha alisema uwepo wa Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) unaongeza fursa za usafirishaji wa mafuta endapo ugunduzi wa kibiashara utafanyika katika eneo hilo.

“Mafanikio tunayoyaona leo yanatokana na uwekezaji mkubwa ambao TPDC imeufanya katika kujenga wataalamu wake. Kwa sasa Shirika lina uwezo mkubwa wa kuendesha na kusimamia shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia kwa kutumia wataalamu wake wenyewe,” alisema Sefue.

Aliongeza kuwa Bodi ya Wakurugenzi imeridhishwa na utendaji kazi wa wataalamu wa TPDC pamoja na mkandarasi AGS kwa namna wanavyotekeleza mradi huo kwa weledi na ufanisi.

Kwa mujibu wa Sefue, mradi huo kwa sasa uko katika hatua ya kijiofizikia ambapo ukusanyaji wa taarifa za mitetemo katika eneo la kilomita 779 umefikia asilimia 78 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2026.

Alisema tafsiri za awali za taarifa hizo zinaonesha viashiria chanya vya uwezekano wa kuwepo kwa mafuta katika eneo hilo.

Akizungumzia masuala ya mazingira, Meneja wa Mradi wa Eyasi Wembere, Sindi Maduhu, alisema mradi umeendelea kuzingatia viwango vya afya, usalama na mazingira kwa kushirikiana na wataalamu kutoka TPDC, Tanzania Fisheries Research Institute pamoja na mamlaka nyingine husika.

Maduhu alisema hadi sasa hakuna madhara hasi ya kimazingira yaliyobainika katika maeneo yanayozunguka mradi huo na kwamba mradi umepata kibali cha kuendelea na utekelezaji kutoka National Environment Management Council.

Aidha alisema mradi huo umechangia kutoa ajira kwa wananchi kati ya 1,500 hadi 1,800 katika kazi mbalimbali pamoja na kuwajengea uwezo wa kitaalamu unaoweza kutumika katika miradi mingine ya mafuta na gesi nchini.

Mpangilio