WAZIRI WA NISHATI AZINDUA SHULE YA BILIONI 1.2 YA LIKONG’O, WANAFUNZI 400 KUNUFAIKA

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amezindua rasmi Shule ya Awali na Msingi ya Likong’o iliyopo mkoani Lindi, iliyojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.2 kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaotekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kushirikiana na kampuni za Shell na Equinor, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mradi wa Kusindika Gesi Asilia kuwa Gesi Asilia Kimiminika (LNG).
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Homera amesema Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa maendeleo ya sekta ya nishati yanaambatana na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wanaozunguka miradi mikubwa ya kimkakati. Amesema ujenzi wa shule hiyo ni mfano wa utekelezaji wa dhamira hiyo kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii inayotekelezwa na TPDC na washirika wa Mradi wa LNG.
“Nimeelezwa na kujionea mwenyewe kuwa mradi huu umekamilika kwa asilimia 100, ukiwa umezingatia viwango vya ubora, usalama na masharti ya kimkataba. Shule hii iliyojengwa kisasa itahudumia wanafunzi takribani 400, wakiwemo wanafunzi 350 wa shule ya msingi na 50 wa shule ya awali, kwa kutoa mazingira bora ya kujifunzia yanayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza kiwango cha ufaulu,” amesema Dkt. Homera.
Shule hiyo ina madarasa tisa, yakiwemo saba ya elimu ya msingi na mawili ya elimu ya awali, pamoja na jengo la utawala, nyumba mbili za walimu, vyoo, vyumba vya stoo, matanki 12 ya kuhifadhia maji na samani za shule. Aidha, miundombinu yake imezingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, ikiwemo vyoo maalumu na njia zinazowezesha upatikanaji wa huduma kwa urahisi.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TPDC, Mha. Paschal Njiko, amesema mafanikio ya miradi ya mafuta na gesi asilia hayapaswi kupimwa kwa thamani ya rasilimali zinazozalishwa pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo endelevu katika jamii zinazozunguka miradi hiyo.
Ameeleza kuwa ujenzi wa shule hiyo umefanikishwa kwa ushirikiano kati ya TPDC, Shell na Equinor, ambapo TPDC imechangia asilimia 26.68 ya gharama za mradi, huku Shell na Equinor kila moja ikichangia asilimia 36.66. Ujenzi ulianza Julai 2025 na umekamilika kwa asilimia 100.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amesema Serikali inaendelea na majadiliano na maandalizi ya kuhakikisha Mradi wa LNG unaanza kutekelezwa mapema iwezekanavyo, huku ikilinda maslahi ya Taifa na kuhakikisha wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla wananufaika na mradi huo.
Uzinduzi wa shule hiyo unaonesha namna ushirikiano kati ya Serikali, TPDC na wawekezaji unavyoweza kuunganisha maendeleo ya sekta ya nishati na huduma muhimu za kijamii. TPDC itaendelea kushirikiana na wadau wake kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia unaleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.




