DEPUTY MINISTER OF ENERGY VISITS MADIMBA NATURAL GAS PROCESSING PLANT

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ametembelea Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba, mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi yenye lengo la kujionea na kufahamu kwa kina miundombinu inayotumika katika uchakataji wa gesi asilia nchini.
Akiwa katika kituo hicho, Mhe. Makamba amekagua miundombinu mbalimbali ya uchakataji wa gesi asilia na kupata maelezo kuhusu mchakato wa gesi asilia kuanzia inapopokelewa, kuchakatwa na kuandaliwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali nchini.
Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia Madimba ni miongoni mwa miundombinu muhimu ya gesi asilia inayomilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kuendeshwa na kampuni tanzu ya Shirika, Gas Company (T) Limited (GASCO).
Kituo hicho kina nafasi muhimu katika kuwezesha gesi asilia inayozalishwa nchini kuchakatwa na kusambazwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa umeme, shughuli za viwanda na matumizi mengine ya kiuchumi.
Ziara hiyo imefanyika wakati Serikali kupitia TPDC ikiendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu ya gesi asilia nchini, ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Ntorya hadi Madimba.
Bomba hilo linatarajiwa kuunganisha gesi asilia kutoka eneo la Ntorya na Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia Madimba, hatua inayolenga kuwezesha gesi hiyo kuchakatwa na hatimaye kutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Ziara ya Mhe. Makamba katika Kituo cha Madimba ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufuatilia maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia pamoja na kuendelea kuimarisha matumizi ya rasilimali hizo katika kuchochea maendeleo ya Taifa.




