WAZIRI MKUU AIPONGEZA TPDC KWA JUHUDI ZA USAMBAZAJI WA NISHATI SAFI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), amelipongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa juhudi zake katika kuhakikisha wananchi wa mikoa mbalimbali nchini, hususan Kanda ya Ziwa, wananufaika na nishati safi ya gesi asilia.
Akizungumza katika banda la TPDC kwenye Kongamano la 4 la Tathmini, Ufuatiliaji na Mafunzo linalofanyika mkoani Mwanza, Mhe. Majaliwa amesema hatua zinazochukuliwa na TPDC zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuwafikia wananchi wote kwa usambazaji wa nishati ya gesi asilia, ambayo ni mbadala wa nishati zisizo rafiki kwa mazingira.
Katika kongamano hilo, TPDC imefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa, zikiwemo; nishati safi ya gesi asilia kwa matumizi ya majumbani, viwandani na kwenye magari.
TPDC ilitumia jukwaa hilo kuelezea fursa mbalimbali za miradi mipya ya gesi asilia inayotarajiwa kutekelezwa nchini, ikiwemo mipango ya kuongeza usambazaji wa miundombinu ya gesi kwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Aidha, miradi hiyo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali ya gesi asilia, kwa lengo la kuimarisha uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.