Tanga Kuwa Kitovu cha Nishati cha Kikanda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, leo wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Kampuni ya Vitol Bahrain kuhusu kuendeleza Mkoa wa Tanga kuwa Kitovu cha Nishati cha Kikanda.
Hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam. Kwa niaba ya TPDC, Hati hiyo imesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika, Bw. Mussa Makame, huku UNOC ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bi. Proscovia Nabbanja, na Vitol Bahrain ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Tom Baker.
Makubaliano hayo yanaweka msingi wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania, Uganda na sekta binafsi katika kuendeleza miundombinu ya mafuta na gesi, kukuza biashara ya nishati na kuifanya Tanga kuwa kitovu muhimu cha huduma za nishati kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Hatua hiyo pia inaendana na dhamira ya TPDC ya kuendeleza rasilimali za petroli kwa manufaa ya Taifa, kuchochea uwekezaji, kuongeza thamani ya rasilimali za mafuta na gesi, pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji wa nishati katika ukanda huu.




