TANZANIA YAGUNDUA GESI ASILIA BILIONI 223 KATIKA KITALU CHA MNAZI BAY

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ametangaza ugunduzi mpya wa gesi asilia unaokadiriwa kuwa futi za ujazo bilioni 223 katika Kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara. Ugunduzi huo umefanyika kupitia ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni ya Maurel & Prom (M&P), ukiwa ni hatua muhimu katika kuongeza rasilimali za gesi asilia na kuimarisha usalama wa nishati nchini.
Ugunduzi huo umehusishwa na kisima cha utafiti cha Kasa-1X ST2, kinachokadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha takribani futi za ujazo milioni 30 za gesi asilia kwa siku kwa kipindi cha angalau miaka 10. Aidha, visima vingine viwili, MB-5 na MS-2, vinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 65 kwa siku, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa matumizi mbalimbali nchini.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa ugunduzi huo, Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Homera, amesisitiza kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi na viwanda nchini unaongeza mahitaji ya nishati, hivyo kuhitaji uwekezaji na juhudi zaidi katika kuendeleza rasilimali za nishati zilizopo nchini.
“Ni ukweli usiopingika kwamba kasi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali nchini, ikiwemo viwanda, ni kubwa. Hali hii inachochea ongezeko kubwa la mahitaji ya nishati kwa ajili ya kuzalisha umeme na matumizi mengine ya viwandani na majumbani. Matarajio ya Watanzania yamebadilika na kwa kiasi kikubwa wanahitaji nishati safi, salama, himilivu na ya uhakika,” amesema Dkt. Homera.
Ugunduzi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa gesi asilia nchini na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi. Pia, unaimarisha nafasi ya gesi asilia katika kusaidia uzalishaji wa umeme, shughuli za viwanda na matumizi mengine ya kiuchumi, sambamba na juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo ya Taifa.
Kupitia ushirikiano na wawekezaji, TPDC inaendelea kutekeleza jukumu lake la kutafuta, kuendeleza na kusimamia rasilimali za mafuta na gesi asilia kwa manufaa ya Watanzania, huku ikichangia katika kuimarisha usalama wa nishati na kukuza uchumi wa Taifa.




