TPDC YAANZA SURA MPYA YA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA, YAPATIWA LESENI NNE

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limepiga hatua muhimu katika kuimarisha ushiriki wake wa moja kwa moja katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia, baada ya Serikali kusaini leseni nne za utafutaji katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara.
Hafla ya utiaji saini wa leseni hizo imefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ikishuhudiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ndejembi amesema hatua ya TPDC kupatiwa leseni hizo inalenga kuimarisha uwezo wa Shirika kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mafuta na gesi asilia, badala ya kutegemea zaidi nafasi ya mshirika katika miradi ya utafutaji na uzalishaji.
Amesisitiza umuhimu wa TPDC kuimarisha uwezo wa wataalamu wake, usimamizi wa miradi na matumizi bora ya mitaji, huku shughuli za utafutaji zikitekelezwa kwa kuzingatia sheria, masharti ya leseni, usalama na utunzaji wa mazingira.
Kupitia leseni hizo, TPDC itaweza kuendesha shughuli za utafutaji kwa kutumia uwezo wake wa kitaalamu na kitaasisi, ama kwa kujitegemea au kwa kushirikiana na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha na kiteknolojia.
Makamu wa Rais ameielekeza TPDC kujenga ushirikiano wenye tija na wawekezaji hao ili kuongeza ufanisi katika utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia, kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ameiagiza Wizara ya Nishati, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kuandaa mpango mkakati utakaowawezesha vijana na kampuni za Kitanzania kunufaika na fursa za ajira, zabuni, mafunzo, teknolojia na uwekezaji katika sekta hiyo.
Amesisitiza kuwa Watanzania, hususan vijana na wanawake, wanapaswa kuandaliwa mapema ili kuwa na ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ya mafuta na gesi asilia.
Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Nishati kuimarisha mifumo ya tathmini, ufuatiliaji na usimamizi wa leseni hizo, kuhakikisha uwajibikaji, nidhamu ya matumizi ya fedha na kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa Taifa.
Utafutaji katika vitalu hivyo unatarajiwa kuongeza taarifa za kijiolojia na kijiofizikia zitakazosaidia kubaini uwepo na ukubwa wa rasilimali zinazoweza kupatikana, na hivyo kuweka msingi wa uwekezaji katika hatua zinazofuata za uendelezaji.
Endapo rasilimali zitagunduliwa na kuthibitishwa kuwa na uwezo wa kuendelezwa kibiashara, zinatarajiwa kuchangia kuongeza upatikanaji wa nishati, mapato ya Serikali, ajira na fursa za kiuchumi kwa Watanzania.
Hatua hiyo inaashiria mabadiliko muhimu katika nafasi ya TPDC kutoka kushiriki zaidi kama mbia katika shughuli za utafutaji hadi kuwa mmiliki wa leseni zake za utafutaji, sambamba na dhamira ya Serikali ya kuimarisha usalama wa nishati, kuongeza ushiriki wa Taifa na kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi.




