TPDC KIFUA MBELE TUZO ZA UBORA WA UANDAAJI NA UWASILISHAJI WA TAARIFA ZA FEDHA 2025

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeibuka mshindi wa Tuzo za Ubora wa Uandaaji na Uwasilishaji wa Taarifa za Fedha kwa Mwaka 2025, katika hafla iliyoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) na kufanyika usiku wa Novemba 26, 2026, katika viwanja vya APC, Mbweni, Dar es Salaam.
TPDC imepata ushindi katika kundi la Mashirika ya Kibiashara Yanayomilikiwa na Serikali, hatua inayotambua ubora wa Shirika katika uandaaji na uwasilishaji wa taarifa zake za fedha. Tuzo hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Nsubili Joshua, na kupokelewa kwa niaba ya TPDC na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC, Mkurugenzi Mrisho Mrisho.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue, amesema kutambuliwa kwa Shirika hilo ni faraja kwa Bodi, kwa kuwa kunathibitisha juhudi zinazoendelea kuhakikisha TPDC inaendeshwa kwa kuzingatia misingi bora ya utawala bora, uwazi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa fedha.
Amesema TPDC ni Shirika la Taifa la Mafuta (National Oil Company) lenye majukumu makubwa katika sekta ya mafuta na gesi, hivyo ni muhimu kuhakikisha taarifa zake za kifedha zinaandaliwa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kimataifa, hususan kutokana na ushirikiano wake na kampuni mbalimbali za kimataifa.
Ameeleza kuwa taarifa za fedha ni sehemu muhimu ya kuonesha taswira ya shirika, kwa kuwa zinaweka wazi namna linavyosimamia rasilimali zake na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sera na miongozo ya Serikali.
Aidha, amesema tuzo za NBAA zina mchango mkubwa katika kuhamasisha ushindani chanya miongoni mwa taasisi, kwa kutambua zinazofanya vizuri katika uandaaji wa taarifa za fedha na kuzichochea nyingine kuboresha mifumo ya usimamizi na uendeshaji.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa TPDC, Francis LUpokela, amesema tuzo hizo zimeongeza morali kwa wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia misingi bora ya usimamizi wa fedha.
Lupokela amesema mafanikio hayo yanaimarisha pia uaminifu wa wananchi kwa TPDC, kwa kuwa ni shirika la umma linalotekeleza majukumu yake kwa kutumia rasilimali za umma, ikiwemo fedha zinazotokana na kodi na tozo mbalimbali.




