TPDC Yakabidhi Gawio la Zaidi ya TZS Bilioni 15.1 kwa Serikali

Dar es Salaam, Julai 2, 2026 – Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekabidhi gawio la TZS 15,118,239,486 kwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya TZS bilioni 3.4 ikilinganishwa na gawio la TZS 11,714,451,625.13 lililowasilishwa katika mwaka wa fedha 2024/25.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika hafla ya Siku ya Gawio 2026 iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hafla hiyo imezikutanisha mashirika na taasisi mbalimbali za umma zilizowasilisha gawio na michango yao kwa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Ongezeko hilo la gawio linaonesha kuendelea kuimarika kwa utendaji wa TPDC pamoja na mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali kupitia usimamizi, uendelezaji na matumizi endelevu ya rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini.
TPDC inaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya utafutaji, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za mafuta na gesi asilia, sambamba na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika sekta mbalimbali za uchumi. Jitihada hizo zinalenga kuimarisha usalama wa nishati nchini, kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha mchango wa sekta ya nishati katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Shirika linaendelea kuongeza ufanisi katika shughuli zake ili kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi zinazalisha thamani kubwa zaidi kwa Taifa na kuwanufaisha Watanzania wa kizazi cha sasa na kijacho.




