TPDC YASHIRIKI MKUTANO WA KUTATHMINI SOKO LA USAMBAZAJI WA GESI ASILIA MIJINI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, limekutana na wawekezaji na wadau mbalimbali katika mkutano wa kutathmini soko la usambazaji wa gesi asilia mijini nchini Tanzania, uliofanyika katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kupata maoni na mtazamo wa wawekezaji kuhusu hali ya biashara ya gesi asilia nchini, fursa zilizopo, changamoto zinazoweza kujitokeza pamoja na mazingira yanayohitajika ili kuongeza uwekezaji katika usambazaji na matumizi ya gesi asilia mijini.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Biashara ya Petroli wa TPDC, Mha. Emmanuel Gilbert, ameeleza hatua zilizofikiwa katika matumizi ya gesi asilia nchini, akibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina vituo 22 vya kujaza gesi asilia iliyogandamizwa (CNG). Amesema ongezeko la matumizi ya gesi asilia linaendelea kuibua mahitaji makubwa ya miundombinu ya usambazaji, hivyo kuwepo kwa fursa kwa wawekezaji kushiriki katika ujenzi na uendeshaji wa miundombinu hiyo ili kuongeza upatikanaji wa gesi asilia kwa wananchi, taasisi, viwanda na vyombo vya usafiri.
Mha. Gilbert amesisitiza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta ya gesiasilia, hususan katika usambazaji wa gesi mijini, na amewakaribisha wawekezaji kutumia fursa hiyo kushirikiana na Serikali kupitia TPDC. Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu, kupanua wigo wa matumizi ya gesi asilia na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na rasilimali hiyo inayopatikana nchini.
Fursa hizo zinaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inasisitiza kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa. Dira hiyo inaweka mkazo katika kujenga uchumi shindani, wenye tija na unaotumia ipasavyo rasilimali za Taifa, sambamba na kuimarisha mazingira ya uwekezaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia. Katika muktadha huo, uwekezaji katika sekta ya gesi asilia unatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayochangia kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa, kukuza shughuli za uzalishaji na kuchochea maendeleo ya viwanda na ajira.
Mkutano huo umeiwezesha TPDC kupata maoni kutoka kwa wawekezaji kuhusu mazingira ya biashara ya gesi asilia nchini, huku ukitoa fursa ya kujadili namna bora ya kuendeleza usambazaji wa gesi asilia mijini kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Kupitia majadiliano hayo, TPDC imeendelea kuwaalika wawekezaji kushirikiana na Serikali katika kutumia fursa zilizopo katika sekta ya gesi asilia, kwa lengo la kuongeza matumizi ya rasilimali hiyo, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuchangia utekelezaji wa azma ya Tanzania ya kujenga uchumi imara na shindani kuelekea mwaka 2050.




