>
emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
ega Logo
Habari
svg-tree

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Ghafi kutoka Ntorya hadi Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba, Mtwara, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika Wilaya ya Mtwara, Kata ya Nanguruwe, ambapo hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 78. Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC pamoja na viongozi na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa mradi.

Mradi huo unagharamiwa na kusimamiwa kwa asilimia 100 na TPDC, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Shirika hilo katika kuongeza uwezo wa uzalishaji na upatikanaji wa gesi asilia nchini. Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 34.2 litasafirisha gesi ghafi kutoka visima vya Ntorya hadi Madimba kwa ajili ya kuchakatwa na kuingizwa katika mfumo wa matumizi ya gesi asilia.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Ndejembi amelipongeza TPDC kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo, pamoja na jitihada za Shirika katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii katika maeneo yanayozunguka mradi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC ameeleza kuwa Shirika linaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuhakikisha unakamilika kwa wakati, huku akibainisha kuwa mradi unatarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 ifikapo Januari 2027.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza kiwango cha gesi asilia kinachozalishwa nchini na kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa umeme, shughuli za viwanda na matumizi mengine ya kiuchumi.

Mradi wa Ntorya–Madimba ni sehemu ya jitihada za TPDC katika kuendeleza rasilimali za gesi asilia nchini na kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kuongeza upatikanaji wa nishati na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Mpangilio