Category Archives: TPDC Blog

Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa TPDC Bi. Marie Msellemu akikabidhi hati ya makabidhiano ya Kambi Namba 8 kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa Dr. Khalfan Ilekizemba.

TPDC YAKABIDHI KAMBI NAMBA 8 KWA SERIKALI YA KIJIJI CHA NJIANNE WILAYA YA KILWA

Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa TPDC Bi. Marie Msellemu akikabidhi hati ya makabidhiano ya Kambi Namba 8 kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa Dr. Khalfan Ilekizemba.

Muonekano wa sehemu ya jengo la Kambi ya Kijiji cha Njia nne Wilaya ya Kilwa
Muonekano wa sehemu ya jengo la Kambi ya Kijiji cha Njia nne Wilaya ya Kilwa

 

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii kwa Vijiji na Mitaa inayoguswa na miundombinu ya bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam.  Katika kufikia azma hii TPDC imekabidhi kambi Namba 8 kwa kijiji cha Njia nne Wilayani Kilwa ili Kijiji kiweze kupanga matumizi sahihi ya Kambi hiyo. Kukabidhiwa kwa majengo ya Kambi hayo kunatokana na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya bomba la gesi asilia kutoka Madimba-Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam, hivyo kufanya majengo hayo kutotumika tena kwa shughuli za ujenzi.

Akikabidhi rasmi kambi hiyo kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Njia nne hivi karibuni, Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa TPDC Bi. Marie Msellemu alisema kuwa “Mikoa ya Lindi na Mtwara ni wadau wakubwa katika ustawi wa miundomibinu ya bomba la gesi asilia na tumekuwa tukishirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo na ya kijamii ikiwemo afya, michezo, utawala bora na maji lengo ikiwa ni kudumisha mahusiano mema na kuboresha huduma muhimu za kijamii, na hivyo kuwataka wananchi wa mikoa hii ya kusini kushirikiana na TPDC katika kuilinda miundombinu ya gesi asilia na kwa pamoja kuboresha huduma za jamii’’.

Akiongea katika hafla ya kukabidhi Kambi hiyo, Kaimu Mkurugezi wa Wilaya ya Kilwa Dr. Khalfani alitoa shukrani za dhati kwa TPDC kwa kuwa mdau mkubwa na wa karibu katika shughuli mbalimbali za maendeleo Wilayani Kilwa hasa katika kuboresha sekta ya elimu na afya. ‘Tunalishukuru Shirika la TPDC kwa kutupatia kambi hii ambayo itasaidia Halmashauri na Kijiji kupanga matumizi sahihi katika nyanja ya afya, Shule au nyumba za watumishi wa umma’’. Pia, alisema kuwa tayari kambi hiyo yenye uwezo wa kuchukua kaya/familia 25 imeshaanza kutumika kwa kusaidia makazi kwa waajiriwa wapya wa Halmashauri.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Daktari Khalfani akiwa na jopo la wadau wa maendeleo katika hafla ya kukabidhi kambi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Daktari Khalfani akiwa na jopo la wadau wa maendeleo katika hafla ya kukabidhi kambi.

 

Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Tingi Bw.  Bayani Saidi Mtendakatika kutoa shukrani zake alisema sambamba na TPDC kutoa Kambi hiyo , Serikali ya Kijjji na wananchi kwa ujumla wanawajibu wa kuilinda na kuhakikisha usafi wa mazingira unaimarishwa ili iweze kudumu na kuwa na tija kwa manufaa ya Kijiji. Aidha, alisema kwamba Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya Kijiji ndiyo utakaoamua na kupanga matumizi ya kambi hiyo ikiwa ni pamoja na kupangaKodi/tozo kwa watakaobahatika kuyatumia majengo ya Kambi hiyo. Bw Bayana alitoa wito kwa TPDC na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kusaidia shughuli za maendeleo kijijini hapo kwani Kijiji kinachangamoto kubwa hasa katika Sekta ya elimu na kuweka bayana mapungufu ya vyumba vya madarasa hali inayopelekea wanafunzi kusomea chini ya miti.

Hati ya Makabidhiano ya Kambi Namba 8 kati ya TPDC na Kijiji cha Njia nne, Wilayani Kilwa
Hati ya Makabidhiano ya Kambi Namba 8 kati ya TPDC na Kijiji cha Njia nne, Wilayani Kilwa

 

 

 

 

Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi. Marie Msellemu akikabidhi hundi ya kiasi cha shillingi Milioni 22 kwa Mkuu wa Shule ya Msingi Kinyerezi Mwalimu Mwl. Pendaman Kajiru

TPDC YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA KIJAMII KINYEREZI NA KIBITI

Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi.  Marie Msellemu akikabidhi hundi ya kiasi cha shillingi Milioni 22 kwa Mkuu wa Shule ya Msingi Kinyerezi Mwalimu Mwl. Pendaman Kajiru

Shirika la Petroli  Maendeleo ya Tanzania (TPDC) limeendelea na mchakato wa kuwajibika kwa jamii na kuendelea kuimarisha huduma mbalimbali zinazowagusa wananchi moja kwa moja kama elimu, afya, maji na utawala bora, ambapo kupitia Sera ya uwajibikaji maarufu kama ‘Corporate Social Responsibility’ (CSR), imeweza kutoa kiasi cha shilingi milioni 22 katika Shule ya msingi Kinyerezi Dar es salaam kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Katika hafla ya kukabidhi hundi ya fedha hizo shuleni hapo, Meneja mawasiliano wa TPDC Bi. Marie Msellemu alisema kuwa TPDC ni wadau wa elimu na Shirika linaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Joseph  Pombe Magufuli, katika suala zima la elimu bure na hivyo kuamua kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira tulivu na salama.

“TPDC ni wadau wa elimu, na tulipoletewa maombi ya kuchangia ujenzi wa madarasa katika shule hii ya msingi hapa Kinyerezi hatukusita kwani ni majirani zetu, kwani tumeendeleza falsafa ya ujirani mwema kama tunavyofanya kwa mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo napo tumewekeza miundombinu ya gesi asilia”

Mgeni rasmi wa shughuli ya kukabidhi hundi ya fedha hizo alikuwa Bibi Sophia Mjema, ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Ilala, Bi. Sheila Lukuba. Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu Wilaya, Bi Lukuba  aliishukuru TPDC kwa kuona umuhimu wa kutoa mchango huo katika Shule hio kwa lengo kuu la kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Bi.Sheila Lukuba akihutubia hadhara katika tukio la kukabidhi hundi S/M Kinyerezi.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Bi.Sheila Lukuba akihutubia hadhara katika tukio la kukabidhi hundi S/M Kinyerezi.

“Naipongeza na kuishukuru sana TPDC kwa kuona umuhimu wa kurudisha asilimia kwa jamii inayowazunguka kwa kutoa fedha za kujenga madarasa kwani itapunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa.” alisema Bi. Lukuba.

Hata hivyo, alihamasisha makampuni na taasisi zingine kuiga mfano wa TPDC na kujitokeza kutatua au kupunguza changamoto zilizopo mashuleni ili wanafunzi wasome katika mazingira bora huku pia akisisitiza wanafunzi kujikita katika kusoma ikiwa wadau wanafanya jitihada nyingi ili waweze kupata mazingira bora ya elimu.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hio Mwl. Pendaman Kajiru aliishukuru TPDC kwa mchango wa ujenzi wa madarasa kwani kulingana na idadi ya wanafunzi shuleni hapo mchango huo utapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuahidi kutendea haki fedha hizo kwa  kujenga madarasa yenye hadhi .

“Napenda kushukuru uongozi wa TPDC kwa mchango wa Milioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kwani  tuliwaomba na hawakusita kutusaidia na msaada huu umetatua kero kubwa ya wanafunzi kubanana katika madarasa kwani wanafunzi ni wengi.” Alisema Mwl. Kajiru.

Vilevile, Afisa Elimu wa kata ya Kinyerezi Bi. Mercy Mtei alishukuru uongozi mzima wa TPDC kwa kuwajengea madarasa kwani kulikua na uhaba mkubwa wa madarasa katika shule za kata kinyerezi ambapo alieleza kwamba uhaba wa madarasa ulipelekea idadi ya wanafunzi 90 kutumia darsa kwa siku moja.

Wakati huo huo katika jitihada za kuinua elimu, TPDC ilikabidhi hundi ya kiasi cha shillingi Milioni 10 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Ndg. Gulam Kifu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Bungu “B” Wilayani Kibiti.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Ndg.Gulam Kifu akikabidhiwa hundi ya shilingi Milioni 10 na Meneja Mawasiliano TPDC Bi. MarieMsellemu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji Bungu B.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Ndg.Gulam Kifu akikabidhiwa hundi ya shilingi Milioni 10 na Meneja Mawasiliano TPDC Bi. MarieMsellemu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji Bungu B.

Akizungumza  katika tukio  hilo Ndg. Kifu aliishukuru TPDC kwa mchango waliotoa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya serikali ya kijiji kwani jengo linalotumika sasa ni chakavu na hatarishi kwa usalama wa watumishi. Zaidi pia alisisitiza Kamati ya ujenzi kutumia fedha hizo kwa kazi iliokusudiwa.

 

 

Choo kipya cha Hingawali kilichojengwa kwa udhaminii wa                   
                                                     TPDC

TPDC YATOA MILIONI 56 KUJENGA VYOO MASHULENI MKOANI LINDI

Choo kipya cha Hingawali kilichojengwa kwa udhaminii wa TPDC

Katika hatua za kuhakikisha sekta ya elimu nchini inaimarika, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 56 ili kutatua kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa vyoo unaoukabili Shule za Msingi Mkoani Lindi.

Akitoa ufafanuzi juu ya fedha hizo, Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi.Marie Msellemu alisema kuwa Shule tano za Msingi mkoani Lindi zimepata msaada wa jumla za shilingi milioni 56 kwajili ya ujenzi wa vyoo baada ya kugundua tatizo la vyoo mashuleni mkoani humo huku akitaja shule hizo kuwa ni shule ya Msingi Madangwa, Hingawali, Ng’apa na Mkupama ambazo kila shule ilipewa kiasi cha shilingi Milioni 10 kwajili ya kuboresha vyoo katika shule hizo, huku Shule ya Msingi Kivinje wilayani Kilwa ikipewa kiasi cha shillingi million 16 kwa ajili ya ujenzi wa choo.

Akikabidhi rasmi vyoo hivyo kwa Mamlaka mbalimbali za shule hizo, Januari, 2019, Bi. Msellemu alisema kuwa TPDC inayo Sera Mfuko wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambao unatumika kurudisha kwa jamii kwa maeneo ambayo kuna uwekezaji wa miradi ya TPDC.

“TPDC inao mfuko wa CSR unaotumika kurudisha kwa jamii katika maeneo ambayo miradi ya TPDC inatekelezwa katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dar es salaam, na katika Mkoa wa Lindi tumeweza kuchangia kiasi cha milioni 56, ambapo milioni 16 zilikwenda Kilwa Kivinje kwa masuala ya kujenga vyoo, Madangwa, Hingawali, Mkupama na Ng’apa pia walipewa milioni kumi kila shule kwajili pia ya ujenzi wa vyoo na jumla kukamilika kuwa milioni 56.”

Kwa kupitia mfuko huu wa kurudisha kwa jamii, TPDC imejikita zaidi katika kuboresha huduma za kijamii kwa maana ya elimu, afya, maji na utawala bora. Msukumo wa kuboresha hali ya vyoo katika shule hizi unalenga kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na afya njema na kuweza kusoma katika mazingira bora.

Aliendelea, “Tunategemea watoto wetu kuwa na utamaduni wa kutumia vyoo lakini pia tunaamini tunawajenga katika mazingira ya kujali afya zao jambo ambalo litawawezesha kusoma kwa utulivu lakini vile vile kuwajengea tabia ya kuendeleza usafi hadi majumbani kwao kwa kusisitiza matumizi ya vyoo bora” alisema Bi. Msellemu.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ng’apa, Mwl. Hamis Abdallah, alitoa shukurani kwa TPDC kwa kutoa milioni 10 na kufadhili ujenzi wa choo chenye matundu sita kwajili ya Wanafunzi na matundu mawili kwajili ya Walimu.

“Kwa kipekee, ninaishukuru TPDC kwa kutatua tatizo la vyoo shuleni kwetu kwani wanafunzi hawakua na vyoo bora vya kutumia lakini pia kabla ya hapo, walimu pia walikua hawana vyoo hivyo ililazimika kwenda kutumia vyoo vya nyumba za walimu wanaoishi karibu na shule, lakini kupitia msaada huu wa TPDC, tumeweza kutatua changamoto hii ambayo hatukuweza kupata suluhisho kwa haraka.”

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Shule ya Msingi Madangwa alishukuru TPDC kwa mchango na ufadhili wa vyoo vya matundu nane kilichotatua changamoto ya vyoo shuleni hapo.

“Kutokana na upungufu wa matundu ya vyoo, TPDC waliona ipo sababu ya kutupatia msaada wa ujenzi wa vyoo vya wasichana matundu 8 ambavyo hadi sasa vimeshakamilika na kuanza kutumika tangu 2017” alisema Mwl. Juma Hamisi ambae ni Mkuu wa Shule ya Msingi Madangwa.

Aidha, kwa upande mwingine, mwanafunzi wa shule ya Madangwa Habib Issa akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, aliishukuru TPDC na kuelezea faida walizopata kwa kuboreshewa mazingira ya vyoo shuleni kwao.

“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Shirika la TPDC kwasababu wametuendeleza katika maendeleo ya shule yetu hususani kwa kutujengea choo kwajili ya wavulana na wasichana ambapo sasa vyoo vina hali nzuri tofauti na hapo awali ambapo kulikua na changamoto.”

Akiongea katika mkutano mfupi uliofanyika shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hingawali Mwl.Osbert Mzesse alikiri kuwa uongozi wa shule ulipokea fedha za ujenzi wa vyoo hatua ambayo imeshakamilika na kuanza kutumiwa na wanafunzi. Aidha aliipongeza TPDC kwa hatua ya kuwafadhili shule yao na kuwajengea choo chenye ubora.

“Tunaishukuru sana TPDC kwa ufadhili huu kwani umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la vyoo shuleni hapa” alisema Mwl. Mzesse.

Taarifa ya Mwalimu Mkuu ilieleza kabla ya mradi mwaka 2016, Shule ilikuwa na matundu 8 tu yaliyochakaa na idadi ya wanafunzi ilikua 483 hivyo kuwa na changamoto kubwa ya utumiaji wa vyoo, lakini baada ya mradi huu mwaka 2019 shule ina matundu 16 yanayoweza kuhimili wingi wa wanafunzi kwa sasa shuleni hapo.

Choo kilichokua kinatumika awali Shule ya msingi Hingawali

Choo kilichokua kinatumika awali Shule ya msingi Hingawali

Choo kipya cha Hingawali kilichojengwa kwa udhaminii wa                                                                        TPDC

Choo kipya cha Hingawali kilichojengwa kwa udhaminii wa  TPDC

Katika Wilaya ya Kilwa, Shule ya Msingi Kivinje ni moja ya shule zilizopewa fedha na TPDC kwajili ya ujenzi wa vyoo. Shule hiyo ilipewa kiasi cha shillingi milioni 16 na ujenzi umeshakamilika shuleni hapo ambapo wamejenga vyoo vyenye matundu 20 ikiwa 10 kwa ajili ya Wasichana na 10 kwa ajili ya Wavulana.

Akielezea kuhusu vyoo hivyo, Mkuu wa Shule ya Msingi Kivinje Mwl.Abbas Ngabuma alisema kuwa vyoo hivyo sasa viko katika hatua ya mwisho kukamilika na baada ya muda mfupi wanafunzi wataanza kuvitumia. Aidha, alitoa shukurani kwa TPDC kwa kuona umuhimu wa kuboresha mazingira ya vyoo shuleni kwao

Choo cha awali cha S/M Kivinje

Choo cha awali cha S/M Kivinje

Choo kipya cha S/M Kivinje kilichojengwa kwa                                                             Ufadhili wa TPDC

Choo kipya cha S/M Kivinje kilichojengwa kwa  Ufadhili wa TPDC

Katika kuhitimisha zoezi la kukabidhi rasmi vyoo hivyo, Bi. Msellemu alishukuru uongozi wa shule hizo kwa kutumia fedha hizo kadri ya matumizi yaliyo kusudiwa na ambapo  Shirika limeridhishwa na ubora, na matumizi sahihi yaliyotumika katika kufanikisha ujenzi huo wa vyoo na pia kuahidi kuwa TPDC ipo kwa ajili ya maendeleo ya jamii ambayo ndiyo maendeleo ya Taifa.

 

 

 

1

TPDC YAIMARISHA SEKTA YA ELIMU MKOANI MTWARA

Bi. Marie Msellemu, Meneja Mawasiliano wa TPDC akimkabidhi hundi Mkuu wa Mkoa wa   Mtwara Mh. Bw. Gelasius Byakanwa kiasi cha Tsh,. 13, 258,042 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa Mkoani Mtwara.

Katika jitihada za kutekeleza dhana ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kutekeleza kwa vitendo dhana hii kwa kushiriki katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo Mkoani Mtwara.

Katika tukio la hivi karibuni, TPDC imeweza kumkabidhi Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Mh. Bw. Gelasius Byakanwa hundi ya kiasi cha shilingi milioni kumi na tatu laki mbili hamsini elfu na arobaini na mbili ili kusaidia ujenzi wa darasa moja katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara.

Akiongea katika tukio hilo, Mh. Byakanwa alisema TPDC imefanya jambo kubwa na kuonyesha uzalendo kwa kurudisha kwa jamii, na aliishukuru TPDC kwa kuendelea kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali mkoani Mtwara, husani zile zinazoikumba sekta ya huduma za jamii ikiwemo elimu. Vile vile mkuu wa mkoa alitoa rai kwa wadau na wawekezaji waliopo mkoani Mtwara kuiga mfano wa TPDC katika kuwajali wananchi kwa kuchangia katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akimkabidhi mfano wa hundi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Bi. Marie Msellemu ambaye ni Meneja Mawasiliano wa Shirika alisema “TPDC ni mdau mkubwa wa Mkoa wa Mtwara, na kwa kupitia mfuko wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), TPDC imekuwa ikiwashika mkono wananchi wa Mkoa wa Mtwara na mikoa ya jirani katika kuboresha huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji na hivyo kiasi hiki cha fedha kitauwezesha mkoa kuendelea kufikia lengo la kuweka mazingira mazuri ya kusomea kwa watoto wetu”.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Ndg. Omari Kipanga alieleza kuwa “Sisi kama halmashauri tumefarijika sana kwa msaada huu uliotolewa na TPDC, kwani fedha hizi zitaelekezwa moja kwa moja katika ujenzi wa madarasa katika halmashauri ya Wilaya yetu kama ilivyokusudiwa. Mchango huu uliotolewa na TPDC unakwenda kukamilisha kazi ya kuezeka madarasa manne katika shule ya msingi Mitambo pamoja na madarasa mawili katika shule ya sekondari ya Madimba’’.

Mkurugenzi Kipanga aliendelea kusisitiza kwamba uhitaji bado ni mkubwa kuweza kukamilisha uhitaji wa madarasa kwa Mkoa wa Mtwara na kuwataka wadau wa elimu na wawekezaji mbalimbali waliopo mkoani Mtwara kuiga mfano wa TPDC katika kurudisha kwa jamii na kuimarisha elimu mkoani hapo.

2

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Ndg.Omari Kipanga akitoa ufafanuzi wa mahitaji ya elimu mkoani Mtwara.

 Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Ndg. Evod Mmanda naye aliungana na viongozi waliotangulia kwa kuishukuru na kuipongeza TPDC kwa kusaidia kuboresha huduma mbali mbali za kijamii mkoani Mtwara. Alieleza kuwa “Si mara ya kwanza kwa TPDC kuchangia kwani mwaka jana tumepokea kiasi cha 21,151,500 za kumalizia ujenzi wa zahanati ya kijjiji cha Mngoji pamoja na kiasi cha 12,000,000 za ujenzi wa choo cha wanafunzi wenye uhitaji maalumu katika shule ya msingi Shangani”.

Katika hatua nyingine TPDC ilikabidhi Taasisi ya Kusaidia Wanawake Mkoani Mtwara (TAKUWA) kiasi cha milioni tatu laki tisa na elfu sabini kwa ajili ya unununuzi wa vitendea kazi vya ofisi ili kurahisisha shuguli za kila siku za taasisi hiyo.

Mratibu wa taasiis hiyo Bi. Hadija Malibecha alishukuru TPDC kwa msaada huo na alieleza kuwa “kabla ya upatikanaji wa vifaa hivyo tulikua tunafanya kazi katika mazingira magumu lakini sasa TPDC imetuboreshea mazingira ya kazi na kazi zinaenda vizuri”. TAKUWA inasaidia vikundi vya wanawake kwa ajili ya kuinua shughuli mbalimbali za kiuchumi na elimu. Jumla ya vikundi 12 vya wakinamama mkoani mtwara vinasimamiwa na taasisi hii katika kupewa mafunzo ya ujasiriamali kama kutengeneza sabuni, ufugaji wa nyuki na ufugaji wa wa mbuzi lengo ikiwa ni kuboresha maisha ya wanawake.

3

Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi. Marie Msellemu akikabidhi hundi kwa mratibu wa taasis ya TAKUWA Bi. Hadija Malibecha

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mha. Kapuulya Musomba (mwenye overall ya bluu) akijadiliana jambo na Ndg. Ildefons Mnimbo ambaye ni mtaalamu kutoka kampuni ya Plasco anaesimamia zoezi la kuunganisha mabomba, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara na lile la kutoka Ubungo kuelekea Mikocheni.

Utekelezaji wa mradi wa kuunganisha gesi asilia kwa matumizi ya majumbani washika kasi

Dar es Salaam, 30 Julai 2018

Ni miezi mitatu sasa tangu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alipozindua rasmi mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi asilia linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam na bomba la kipenyo kidogo linalotoka Ubungo kuelekea Mikocheni. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mha. Kapuulya Musomba alifafanua kwamba utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza matumizi ya gesi asilia kwa jiji la Dar es Salaam kwa kuwaunganisha wateja zaidi wa matumizi ya majumbani na viwandani.

Mradi huu unahusisha ujenzi wa msingi kwa ajili ya kusimika mtambo wa kupunguza mgandamizo, uunganishaji wa vipande vya mabomba, kuthibitisha njia ya bomba, uchimbaji na ulazaji wa bomba litakalochukua gesi kutoka bomba kubwa, uwekaji wa viainisho vya bomba linapopita na ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu kuvuka mto Ubungo. Akizungumza juu ya hatua za utekelezaji, Meneja Mradi Ndg. Denice Byarushengo alisema “mradi umepiga hatua kubwa na muhimu ambapo hadi sasa ujenzi wa msingi kwa ajili ya kusimika mtambo wa kupunguza mgandamizo umekamilika kwa asilimia 97%, uthibitisho wa njia ya bomba na zoezi la kuchimba mitaro kwa ajili ya mabomba umekalimilika kwa asilimia 76.8%, uunganishaji wa mabomba umekamilika kwa asilimia 88.6%, ulazaji na ufukiaji wa mabomba umekamilika kwa asilimia 56.9%, viainisho sita (6) vya bomba linapopita vimeshawekwa na ujenzi wa dara la waenda kwa miguu umekamilika kwa asilimia 90%”. Aidha, Meneja Mradi aliongeza kwamba utekelezaji wa mradi huu unahusisha kuvuka mto Ubungo pamoja na barabara ya Ubungo Maziwa na ya Mandela ambapo hadi sasa kazi ya kuvuka mto Ubungo imekamilika kwa asilimia 100% na ile ya kuvuka barabara ya Ubungo Maziwa imekamilika kwa asilimia 50% wakati ya kuvuka barabara ya Mandela ikiwa mbioni kuanza.

Bomba lenye kipenyo cha 315mm likiwa limelazwa katika mtaro tayari kufukiwa, hii ni sehemu ya bomba linalochukua gesi asilia kutoka kwenye bomba kuu linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kuunganisha na bomba linalotoka Ubungo kuelekea Mikocheni.
Bomba lenye kipenyo cha 315mm likiwa limelazwa katika mtaro tayari kufukiwa, hii ni sehemu ya bomba linalochukua gesi asilia kutoka kwenye bomba kuu linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kuunganisha na bomba linalotoka Ubungo kuelekea Mikocheni.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mha. Kapuulya Musomba ambaye alifanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo hapo jana alionyesha kuridhishwa na kazi na ubora wa utekelezaji wa mradi, Mha. Kapuulya alisema “pamoja na changamoto zilizopo, ninayo furaha kwamba kazi zinafanyika kwa kasi na ubora wa hali ya juu na ni matumaini yangu baada ya kuongea na mkandarasi pamoja na msimamizi wa mradi kwamba mradi utamalizika ndani ya wakati”.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mha. Kapuulya Musomba (mwenye overall ya bluu) akijadiliana jambo na Ndg. Ildefons Mnimbo ambaye ni mtaalamu kutoka kampuni ya Plasco anaesimamia zoezi la kuunganisha mabomba, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara na lile la kutoka Ubungo kuelekea Mikocheni.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mha. Kapuulya Musomba (mwenye overall ya bluu) akijadiliana jambo na Ndg. Ildefons Mnimbo ambaye ni mtaalamu kutoka kampuni ya Plasco anaesimamia zoezi la kuunganisha mabomba, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara na lile la kutoka Ubungo kuelekea Mikocheni.

Mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi asilia na lile la Ubungo kuelekea Mikocheni lenye urefu wa kilomita 7.8 na uwezo wa kusafirisha gesi kiasi cha futi za ujazo milioni 7.5 kwa siku unalenga kuunganisha kiwanda cha Coca Cola Kwanza Ltd na BIDCO pamoja na wateja takribani 1000 wa majumbani ambao wataunganishwa kwa awamu. Mradi huu utawezesha upatikanaji wa gesi asilia ya kutosha katika bomba litokalo Ubungo kuelekea Mikocheni kupitia barabara ya Sam Nujoma kusambaza gesi kwa wateja wa majumbani katika maeneo ya Ubungo, Shekilango, Mlalakuwa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sinza na Mikocheni. Mkandarasi wa mradi huu ni kampuni ya SINOMA kutoka Jamhuri ya Watu wa China na mradi unagharimu shilingi za kitanzania bilioni 4.2 ambazo ni fedha za ndani kutoka TPDC. Vile vile mradi huu unatoa fursa kwa kampuni za wazawa kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuza bidhaa za ujenzi kama vile mabomba ambapo kwa sasa kampuni ya Plasco ndio mshindi zabuni hiyo. Mkandarasi wa mradi pia ana fursa ya kutoa kazi kwa mkandarasi mwingine (sub-contracting) lengo likiwa ni kuchochea ushirikishwaji wa wazawa katika sekta ya mafuta na gesi hapa nchini.

Sehemu ya eneo la barabara ya Ubungo Maziwa inayochimbwa kitaalamu bila kuvunja barabara ili kuruhusu bomba la gesi kuvuka barabara hiyo.
Sehemu ya eneo la barabara ya Ubungo Maziwa inayochimbwa kitaalamu bila kuvunja barabara ili kuruhusu bomba la gesi kuvuka barabara hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba akieleza kwa kina Mradi Mpya wa Kuunganisha gesi asilia kutoka bomba kubwa hadi kwenye bomba dogo la Ubungo Mikocheni mradi ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi miezi miwili

Matumizi ya gesi asilia yazidi kushika kasi

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba akieleza kwa kina Mradi Mpya wa Kuunganisha gesi asilia kutoka bomba kubwa hadi kwenye bomba dogo la Ubungo Mikocheni mradi ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi miezi miwili

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekabidhi mradi wa uunganishaji wa gesi asilia kutoka katika bomba kubwa la gesi asilia linalomilikiwa na TPDC kwenda kwenye bomba dogo la usambazaji wa gesi asilia kutoka Ubungo hadi Mikocheni ambalo nalo linamilikiwa na TPDC ili kuongeza kiasi cha gesi asilia katika bomba hilo kwa lengo la kuwafikia watumiaji wengi zaidi.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba akikabidhi jukumu la ujenzi wa mradi wa uunganishwaji wa gesi asilia kutoka kwenye bomba kubwa la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam katika eneo la Valvu namba 15 (Block Valve Station-BVS) ambapo ndipo bomba hilo litarajiwa kujengwa hadi eneo la Ubungo Maziwa litakapounganishwa na bomba dogo la usambazaji wa gesi asilia kuelekea Mikocheni Dar es Salaam.

“Leo ni siku kubwa sana kwetu kama Kampuni ya Mafuta ya Taifa tunapokabidhi rasmi jukumu la ujenzi wa miundombinu ya kutoa gesi asilia kutoka kwenye bomba letu kubwa kwenda kwenye bomba letu dogo la usambazaji wa gesi asilia kazi ambayo itafanywa na kampuni ya SINOMA ambayo faida yake kubwa ni kulipa uwezo wa kubeba na kusambaza gesi nyingi zaidi itakayoruhusu uunganishwaji zaidi wa gesi asilia kwa watumiaji wapya katika maeneo yote ambayo bomba hilo linapita yaani Ubungo, Sinza, Chuo Kikuu, Survey, Mwenge na Mikocheni” alifafanua Kaimu Mkurugenzi.

Akizungumzia wanufaika wa mradi huo pindi utakapokamilika, ndugu Musomba amesema kuwa, pamoja na kuendelea kusambaza kwa watumiaji wa zamani ambao ni MM I, MM II, MM III, TanPack na Iron and Steel wateja wapya watakaonufaika ambao tayari wameshakubaliana ni Coca Cola kwanza Limited na BIDCO na nyumba 70 katika awamu ya kwanza na kwamba wanatarajia kuunganisha kwa viwanda zaidi vitakavyokuwa tayari kwa muda wowote.

Aidha akieleza kuhusu utaratibu wa uunganishwaji wa gesi asilia kwa watumiaji Mhandisi Musomba ameeleza kuwa, “Utaratibu ni wa kawaida sana kikubwa mteja tarajiwa anatakiwa kuwasilisha barua ya maombi ya gesi asilia kisha wataalam kufanya utafiti wa namna ya kumuunganishia mteja gesi hiyo na kwa upande wa watumiaji wa majumbani tunashauri pia nyumba kadhaa kuungana pamoja na kuleta barua kisha taratibu za kiutalamu za namna ya kuwafikishia gesi asilia zifanyike.”

Meneja Mkuu Msaidizi wa SINOMA ndugu Lu Xiaoqiang akielza kwa waandishi wa habari namna watakaovyotekeleza ujenzi wa Miundombinu hiyo kwa ufanisi na wakati kadiri ya masharti ya mkataba
Meneja Mkuu Msaidizi wa SINOMA ndugu Lu Xiaoqiang akielza kwa waandishi wa habari namna watakaovyotekeleza ujenzi wa Miundombinu hiyo kwa ufanisi na wakati kadiri ya masharti ya mkataba

Kwa upande wake Meneja Mkuu Msaidizi wa SINOMA ndugu Lu Xiaoqiang ambao ndio Wakandarasi walioshinda zabuni ya ujenzi wa mradi huo amesema kuwa, “Leo ni siku ya furaha kwa kuwa tumeweza kupata nafasi ya kutekeleza mradi wa TPDC wa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka eneo la Ubungo bomba ambalo tunaamini litasaidia kukuza uchumi wa nchi nzuri ya Tanzania kwa kusambaza nishati viwandani na majumbani.”

Akizungumzia gharama za matumizi ya gesi asilia majumbani Mhandisi Musomba amefafanua kuwa, “Matumizi ya gesi asilia ni ya gharama nafuu kulinganisha na mkaa na gesi za mitungi-LPG ambapo kwa mtumiaji wa gesi za mitungi mfano wa Kilo 15 ambayo itatumika kwa mwezi mmoja kama akitumia gesi asilia atatumia hadi miezi miwili na hivyo kuokoa karibu nusu ya gharama ya matumizi ya nishati majumbani lakini pia gesi asilia ni nyepesi kuliko hewa na hivyo kuwa salama zaidi kwa matumizi hata pale inapovuja kwa kuwa hupotea hewani.”

Jukumu la kusambaza gesi asilia ni la msingi kwa maeneo ya uchumi imara wa viwanda na hivyo TPDC inaendelea kufanya tafiti za kitaalamu za usambazaji wa gesi asilia katika maeneo mengine ya nchi yakiwemo Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Dodoma.

DSC_8999

TPDC Limewezesha Uchumi wa Viwanda

Mhandisi wa Uendeshaji wa Bomba la Gesi, Ndugu Hassan Temba akiwaeleza kwa vietendo Wahairi wa Habari namna ambavyo wanaendesha na kusimamia bomba la gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam kwa urahisi zaidi wakiwa kwenye Chumba cha Uendashaji na Usimamizi wa Gesi Asilia Kinyerezi kwa msaada wa vifaa maalum vya mawasiliano vilivyowekwa kwenye mundombinu ya gesi asilia.

“Kukamilika kwa Miundombinu ya Taifa ya kuchakata na  kusafirisha gesi asilia pamoja utafiti wa kina wa gesi asilia uliofanyika na kupelekea kugundua kiasi cha gesi asilia cha futi za ujazo trilioni 57.55 pamoja na utafiti unaondelea kufanyika katika baadhi ya maeneo nchini yakiwemo ya Ruvu na Eyasi Wemberi ni sehemu ya mikakati kabambe ya TPDC katika kuiwezesha Tanzania kujenga uchumi imara na endelevu wa viwanda”

Haya yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Utawala TPDC, Ndugu Hans Mwambuba ambaye alimuwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wakati akifungua warsha ya siku moja kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyobeba mada kuu ya Mkakati wa TPDC kuelekea Tanzania ya Viwanda iliyoifanyika katika Kituo cha Kupokelea Gesi Asilia cha Kinyerezi mwishoni mwa wiki.

Ndugu Hans amewashukuru kwanza wahariri kwa kutoa muda wao na kukubali wito wa kuhudhuria warsha hiyo ya siku moja na kwamba ni matumaini yake na ya shirika kuwa kiu ya kutaka kufahamu kiundani mikakati ya TPDC kuelekea uchumi wa viwanda ndio iliyowafanya wahudhurie semina hiyo kwa lengo la kujijengea uelewa mpana na sahihi wa TPDC na shughuli zake ili waweze kupelekea taarifa sahihi kwa wananchi.

Akiwa anamkaribisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Meneja Mawasiliano wa Shirika hilo ambaye Kitengo chake ndicho kimeandaa na kuratibu Warsha hiyo ameeleza kuwa “Sisi kama Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania tunatambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kuelimisha na kuuhabarisha umma na ndio maana tumekuwa tunafanya warsha kwa wanahabari nchi nzima na leo hii tunayofuraha kuwa nanyi wahariri katika warsha hii yenye lengo kubwa la kuwaongezea ufahamu sahihi wa sekta ya mafuta na shughuli za TPDC na makampuni yake tanzu ya GASCO na TANOIL ili muweze kutoa taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu shughuli za shirika lakini pia sekta ya mafuta kwa ujumla wake”

Akielezea mikakati ya TPDC kuelekea Uchumi wa Viwanda ndugu Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ameeleza kuwa “Matumaini ya kujenga uchumi bora wa viwanda nchini tuliweza kuyaleta mara baada ya kukamilika kwa mitambo ya kuchakata gesi asilia iliyopo Songo Songo mkoani Lindi na Madimba mkoani Mtwara pamoja na bomba kubwa la kusafirishia gesi hiyo hadi Dar es Salaam na kikubwa kwenye miundombinu hii ni kwamba imefungua fursa ya uwekezaji wa viwanda katika mikoa yote iliyopita na hii ni kwasababu muwekezaji ana uwezo wa kuunganishiwa gesi asilia kama nishati ya kuendesha mitambo au kuzalisha umeme wa kutumia kwenye viwanda”

Ameongezea kuwa kutokana na bomba hilo tayari tumeunganisha gesi kwenye kiwanda cha vigae cha Goodwill kilichopo mkoa wa Pwani, tumeshafikisha bomba kwenye kituo cha kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya kiwanda cha saruji cha Dangote vile vile miradi ya kuunganisha gesi asilia katika kiwanda cha Coca Cola, BIDCO na nyumba 67 katika jiji la Dar es Salaam pamoja na kutoboa bomba kuu la gesi asilia katika kijiji cha Mwanambaya kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kwa lengo la kutoa gesi ya kutosha na kusambaza kwenye viwanda vya Mkuranga kwa kuanza na Lodhia na Knauf.

Aidha akisisitiza kwenye kuongeza ugunduzi zaidi wa gesi asilia na mafuta ndugu Hans ameeleza kuwa “Tukiwa Shirika la Mafuta la Taifa pia tumeelekeza mikakati yetu kwenye kuhakikisha tunaongeza kiasi cha ugunduzi wa gesi asilia na pengine mafuta kwa kuendelea kufanya utafiti zaidi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ambapo kama sehemu ya mkakati kwa sasa tuna kitalu cha Eyasi Wembere, Songo Songo Magharibi, Kitalu namba 4/1b na 4/1c na Mnazi Bay Kaskazini pamoja na miradi hii ya kimkakati ambayo inafanywa na Shirika upo pia mradi unaotekelezwa na mwekezaji katika kitalu cha Ruvu ambae anaendelea na kufanya utafiti wa uhakiki wa kiasi cha gesi asilia katika kitalu hicho lengo kuu likiwa tuvuke pale kwenye futi za ujazo trilioni 57.55 zilizopo kwa sasa”

Sehemu ya baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia kwa umakini mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wataalam kutoka TPDC na GASCO ambao waliweza kueleza mikakati ya TPDC katika kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha utafiti zaidi wa mafuta na gesi asilia unafanywa ili kuongeza uwepo wa rasilimali hizo kwa matumzi lakini pia usambazaji wa gesi asilia unafanywa kwa kasi kufikia wateja haswa viwanda
Sehemu ya baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia kwa umakini mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wataalam kutoka TPDC na GASCO ambao waliweza kueleza mikakati ya TPDC katika kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha utafiti zaidi wa mafuta na gesi asilia unafanywa ili kuongeza uwepo wa rasilimali hizo kwa matumzi lakini pia usambazaji wa gesi asilia unafanywa kwa kasi kufikia wateja haswa viwanda

Aidha kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri ndugu Deodatus Balile ameipongeza TPDC kwa kuendesha warsha hiyo ambayo imeongeza uelewa mkubwa wa gesi asilia kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.

“Niwapongeze kwa kuendesha mafunzo haya kwakweli ni muhimu kama mlivyoona kuwa baadhi yetu bado hatuelewi masuala mengi ya sekta hii na ndio maana hata maana ya Mkondo wa Juu na Mkondo wa Chini katika Gesi na Mafuta imekuwa ikileta mkanganyiko kati yetu hivyo mnapaswa mfanye zoezi hili kuwa endelevu ili wahariri na waandishi waelewe haswa kiundani masuala ya mikataba, sheria zinazosimamia sekta hii pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa na TPDC na matumizi na manufaa ya gesi asilia” ameongeza Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri.

Aidha Ndugu Balile ameshauri kuwa TPDC inapaswa kuunda kundi la waandishi wa habari ambao mtawajengea programu maalum ya elimu ya sekta kwa kuwapeleka kwenye maeneo ya uzalishaji, utafiti na uchimbaji pamoja na kuwapa mafunzo ya sheria, mikataba na masuala mengine ya sekta hii ambao hawa watakuwa mabalozi wenu upande wa vyombo vya habari” alifafanua ndugu Balile.

DODSAL DRILING 2

TPDC na jitihada za kulihakikishia Taifa gesi ya kutosha

Moja ya wataalam wa milipuko akipima urefu wa shimo kama limekidhi mahitaji ya kitaalam kabla ya kusimika/kujaza baruti ndani ya shimo.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) akiwammiliki wa leseni za vitalu vya gesi na mafuta nchini kwa kushirikiana na mkandarasi kampuni ya Dodsal wanaendelea kufanya utafiti wa ukusanyaji wa takwimu za mitetemo “2D seismic data” utafiti unahusisha eneo lenye urefu wa takribani km 1287 wa gesi asilia katika Kitalu cha Ruvu kilichopo Mkoa wa Pwani na baadhi ya maeneo ya Dar es salaam kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania inapata gesi asilia au mafuta ya kutosha itakayojenga uchumi imara wa viwanda.

Akielezea umuhimu wa utafiti huo ndugu Simon Kimario ambaye ni Mjiofizikia kutoka TPDC amesema kuwa lengo kuu la utafiti huo nimuendelezo wa utafiti wa mafuta na gesi unaofanywa na mwekezaji Dodsal Hydrocarbons akishirikiana na TPDC katika kitalu cha Ruvu ilikuwezesha kugundua gesi asilia nyingi zaidi na pengine mafuta ilikuhakikisha Taifa linakuwa na chanzo imara   cha nishati ambacho kitalisaidia taifa katika kujenga uchumi wa viwanda.

RAMANI DODSAL

Ramani inayoonyesha kitalu cha utafiti cha Ruvu

DODSAL AVO

Moja ya kitafaa maalumu (AVO) ya kunakili taarifa za mitetemo za kijiofizikia kikiwa kimesimikwa ardhini tayari kusubiri mitego ya baruti kulipuliwa ili kupata taarifa za mitetemo. Mtambo huu hutumika ili kupata taarifa za mitetemo zenye taswira ya pande mbili “2D”.

“Tayari hatua kadhaa zimeishafanyika kama vile; uandaaji wa ramani ya kiutafiti ambayo kazi yake nikuonyesha eneo la kitalu na maeneo muhimu ya kufanyia utafiti, ambapo kunapelekea kwenye hatua nyingine ya kwenda kwenye eneo halisi na kubaini mistaria ambayo taarifa za mitetemo zitachukuliwa, hatua ambayo itanguliwa  na zoezi la kupata vibali na kuelimisha wananchi kuhusu namna zoezi zima na ushirikishwaji wa wananchi utakavyofanyika.”

Akiogelea hatua zinazoendelea sasa hivi ndugu kimario anaeleza kuwa shughuli zinazoendelea katika maeneo tofauti tofauti kwa sasa ni pamoja na usafishaji njia au mistari, kuchimba mashimo ya kina kifupi mita 7, 10 au 15 kutegemea na jiolojia ya eneo kwa ajili ya kuweka baruti (vyanzo vya mitetemo ) pamoja  na kuweka mitambo maalum ya kuchukulia taarifa za mitetemo(seismic data)

DODSAL DRILLING

Mtambo wa kuchoronga mashimo ya kuwekea baruti ukiwa kazini. Mtambo huu huchimba mashimo yenye urefu tofauti kati ya mita 7 hadi 15, kwaajili ya kufukia baruti ambazo zinapolipuliwa ndipo taarifa za miamba chini hupatikana baadae kuchakatwa na kutafsiriwa kitaalam ilikujua sehemu ya kuchimba kisima cha utafiti

Aidha anaeleza kuwa, “Yapo maeneo mengine ambayo yamefikia kwenye hatua ya kubainisha maeneo maalum yatakayowekewa baruti pamoja na vifaa vya kunakili au kunasa taarifa za mitetemo, yapo maeneo ambayo tayari zoezi hili limeshafanyika na tayari hatua ya kulipua baruti na kunakili taarifa za mitetemo limekwishaanza kufanyika”

Ndugu Simon amethibitisha kuwa hadi sasa takribani mashimo yaliyopo kwenye misatri yenye urefu wa km 311 yameishasimikwa au kujazwa na baruti na mistari ya kijiofizikia yenye urefu wa Kilomita 116.9 kati ya 1287 imeshachukuliwa taarifa za kijiofizikia na kuendelea  kufanyiwa uchambuzi wa awali.

Aidha akiongolea suala la vibali na fidia kwa wananchi ambao mazao yao yameathirika na yatakayoathirika na zoezi la uchukuaji wa taarifa za mitetemo , ndugu Mohamed Ally ambaye ni Msimamzi wa Vibali kutoka kampuni ya Envision  Consulting Ltd  ameeleza kuwa kumekuwa na ushirikiano mkubwa sana kutoka TPDC haswa panapohitajika vibali kutoka katika mamlaka mbalimbali za serikali na hivyo kumefanya kazi yao kuwa rahisi na yenye mafanikio.

DODSAL BARUTI

Moja ya baruti zinazofukiwa chini ikiwa kwenye maandalizi ya kufukiwa kwenye shimo maalum kwa ajili ya kulipuliwa.

Akiongolea suala la fidia, ndugu Mohamed anabainisha kuwa “pamoja na kuwa na mtathamini    wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na viongozi kutoka ofisi za Kata, Wilaya, Mikoa pamoja Mthamini  Mkuu wa  wa Serikali na hivyo kufanya zoezi zima la uthamini na ulipaji fidia kufanyika kwa mafanikio makubwa na kupunguza migogoro na wananchi”

Pamoja na utafiti unaofanyika katika kitalu cha Ruvu, TPDC linaendelea na maandalizi ya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini kama vile vitalu vya; Eyasi-Wemberi, Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay kaskazini pamona na Vitalu vya 41B/41C.

 

 

 

 

kinyerezi

TPDC yawezesha kuwashwa mitambo ya Kinyerezi II

Dar es Salaam, 4 Aprili 2018

 

Mwaka 2004 utaendelea kubaki katika kumbukumbu za nchi yetu kama mwaka wa mageuzi katika sekta ya nishati ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia. Miaka kumi na nne baadae, Tanzania imeendelea kuwa kinara katika nchi za Afrika Mashariki ambazo zinatumia gesi asilia kuzalisha umeme ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 50% ya umeme unaozalishwa nchini unatokana na nishati ya gesi asilia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi II, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. John Pombe Joseph Magufuli alisema “nishati ya umeme ni injini na muhimili muhimu katika ukuzaji uchumi na ustawi wa maisha ya binadamu, umeme unachochea shughuli za uzalishaji na hivyo kutoa fursa za ajira na kuboresha maisha ya watu”.  Mh. Rais pia aliongeza “Azma na dhamira yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haiwezi kutimia bila ya kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika”. Mitambo ya kufua umeme ya Kiyerezi II ina uwezo wa kuzalisha megawati 240 za umeme na inategemea gesi asilia inayozalishwa na kusambazwa na TPDC kupitia kampuni tanzu ya Gasco inayosimamia shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa gesi asilia nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alieleza mipango ya Wizara ya Nishati katika kufikia Tanzania ya viwanda kwa kutumia gesi asilia kuzalisha umeme wa uhakika. Dk. Kalemani alisema “ufunguzi wa Kinyerezi II ni muendelezo wa miradi ya umeme wa gesi asilia, baada ya mradi wa leo tunategemea kutekeleza miradi mingine miwili hapa Kinyerezi ambayo yote itatumia gesi asilia na kuzalisha megawati 600, isitoshe tunatarajia kuzalisha umeme wa gesi asilia pale Somangafungu megawati 320 na kule Mtwara megawati 300”. Ni wazi kabisa kwamba mchango wa gesi asilia hususan kwenye upatikanaji wa umeme wa uhakika hapa nchini ni jambo lililo wazi na la kujivunia.

kinyerezi
Sehemu ya Mitambo ya Kituo cha kupokea gesi Asilia Kimyerezi, Kituo hiki ndicho kinachopokea gesi asilia na kuipeleka katika mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi na Ubungo na nyngine kupelekwa katika viwanda

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba alisema “TPDC imejipanga vema kuhakikisha gesi asilia inaendelea kupatikana kwa wingi ili kuwezesha Tanzania ya viwanda sio tu kwenye umeme bali hata kwenye viwanda moja kwa moja ambapo hutumika kama chanzo cha nishati au malighafi”.  Mhandisi Musomba alieleza namna ambavyo TPDC kupitia kampuni tanzu ya Gasco walivyohakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kuwezesha kuwashwa kwa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi II.

TPDC ambalo ni Shirika la Mafuta la Taifa ndio mmiliki wa leseni zote za utafiti na uendelezaji wa gesi asilia na mafuta nchini. Katika kutekekeleza majukumu yake, TPDC huingia mikataba ya kugawana mapato ijulikanayo kama “Production Sharing Agreement (PSA)” na kampuni za kimataifa za mafuta na gesi (IOC) ambazo hujulikana kama mkandarasi. Kazi ya mkandarasi huyu ni kufanya kazi za utafiti na uendelezaji wa mafuta na gesi kwa kushirikiana na TPDC ambapo TPDC husimamia maslahi ya nchi na kuhakikisha tozo zote pamoja na hisa za Serikali katika mikataba hiyo zinalindwa na kulipwa kwa wakati.

cargo

TPDC Invites Bids for X-Ray Cargo Scanners

1. This Invitation for Bids follows the General Procurement Notice (GPN) for this project that appeared in UNDB online: dated 30th November 2017 and on the African Development Bank Group’s Internet Website;

2. The United Republic of Tanzania has received Financing from the African Development Bank in various currencies towards the cost of Institutional Support Project for Domestic Resources Mobilization and Natural Resources Governance (ISP-DRM & NRG). It is intended that part of the proceeds of this loan will be applied to eligible payments under the contract for Supply, Installation and Commissioning of Two (2) X-Ray Portal Scanners.

3. The Tanzania Petroleum Development Corporation on behalf of Tanzania Revenue Authority (TRA) now invites sealed bids from eligible bidders for the Supply, Installation and Commissioning of Two (2) X-Ray Portal Scanners.

4. Interested eligible bidders may obtain further information from and inspect the bidding documents at the office of the Procurement Manager, room number 101 on the 10th floor at Tanzania Petroleum Development Corporation, Head office situated at Benjamin William Mkapa Pension Towers, Tower ‘A’,  Azikiwe/ Jamhuri streets, Dar-es-Salaam from 8.30 to 3.30 pm from Monday to Friday inclusive except on public holidays. See Directions.

5. A complete set of bidding documents in English may be purchased by interested bidders on the submission of a written application to The Managing Director, Tanzania Petroleum Development Corporation, P. O. Box 2774, Dar es Salaam and upon payment of a nonrefundable fee amount of Tshs. 100,000.00/= (Tanzania Shillings One Hundred Thousand only). Payment should be made through CRDB Bank, Account Name: TPDC Main Account, Account Number: 01J1007309500 payable to Tanzania Petroleum Development Corporation.

6. The provisions in the Instructions to Bidders and in the General Conditions of Contract are the provisions of the African Development Bank Standard Bidding Document: Procurement of Goods.

7. Bids must be delivered to the above office on or before 11.00 hours on 09th February, 2018 and must be accompanied by a bid security in the amount of not less than United State Dollars One Hundred Thousand Only (USD 100, 000.00).

8. A mandatory site visit shall be held on Friday 19thJanuary, 2018 at 11:00 Hours local time. Bidders are required to assemble at Port of Dar Es Salaam.

9. Bids will be opened in the presence of bidders’ representatives who choose to attend at 11:00 hours local time on 09th February, 2018 at the offices of Tanzania Petroleum Development Corporation, situated at Benjamin William Mkapa Pension Towers, Tower ‘A’, 10th Floor, Board room number 106, Azikiwe/ Jamhuri streets.

10. Bids must be delivered to the address below by hand or courier by 09th February, 2018 at 11:00 hours and mentioned on the envelope “Supply, Installation and Commissioning of Two (2) X-Ray Portal Scanners”.

 

Attn: Managing Director, Tanzania Petroleum Development Corporation, Benjamin William Mkapa Towers, Tower “A”, Azikiwe/Jamhuri Streets, Room No. 401, 4th Floor, P.O. Box 2774, Dar-es-Salaam, Tanzania. Tel: +255-22 2200103-4, 2200112, Fax: +255-22-2200113. E-mail: tpdcmd@tpdc.co.tz