DSC_3284

TPDC kuwekeza kiwanda cha mbolea Kilwa

Na.1

Mkurugenzi wa uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa gesi kutoka TPDC, Dkt. Wellington Hudson akitoa mada wakati wa semina ya kuwajengea uelewa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa juu ya miradi ya gesi asilia.

DSC_3284

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio

Katika kutekeleza azma ya Serikali kuanzisha viwanda mbalimbali nchini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na Kampuni ya Ferostaal Industrial Project GmbH (wawekezaji kutoka Ujerumani) na washirika wake wameinigia makubaliano (Joint Venture) ya kutekeleza mradi wa mbolea. Mradi huu unalenga kuzalisha tani 3,850 za mbolea kwa siku na utatumia gesi kiasi cha futi za ujazo milioni 104 kwa siku.

Akiongea na Madiwani wa Halmashauri ya Kilwa, Mkurugenzi wa uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji kutoka TPDC, Dkt. Wellington Hudson alisema ujenzi wa kiwanda hiki unalenga kuzalisha aina mbili za mbolea ambazo ni ammonia na urea na uwekezaji wake unatarajiwa kugharimu dola za marekani bilioni 1.9. Dkt. Hudson aliyasema haya wakati wa semina ya kujenga uelewa kwa Madiwani na viongozi wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa juu ya miradi mbalimbali ya gesi asilia inayopangwa kutekelezwa katika Wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio akizungumza katika semina hiyo alisema mradi huu wa mbolea unatarajiwa kutoa ajira takribani 5000 za moja kwa moja, kufungua fursa zaidi za kutoa huduma na kuuza bidhaa kipindi cha ujenzi na hata kipindi cha kutekeleza mradi huu. Vile vile, mradi utaongeza pato kwa Halmashauri kwa uongeza uzalishaji wa gesi asilia na kuboresha huduma mbalimbali kama vile za afya, kiwanja cha ndege, bandari, huduma za afya na nyinginezo nyingi.

Semina hiyo ilihudhuriwa na Madiwani wote wa Wilaya ya Kilwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Kilwa, Wabunge, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mkurugenzi wa Wilaya na Wakurugenzi wengine wa Halmashauri na ililenga kujenga uhusiano na kuboresha mahusiano baina ya TPDC na Wilaya ya Kilwa.

Ugunduzi wa gesi asilia nchini umeendelea kufungua fursa zaidi za uwekezaji na kuendelea kukuza uchumi. Mpaka sasa tayari takribani asilimia 70% ya umeme unaotumika hapa nchini unazalishwa kwa gesi asilia. Kwa mujibu wa taarifa kutoka TPDC tayari viwanda vipatavyo 37 jijini Dar es Salaam vinatumia gesi asilia.