1

TPDC yawakutanisha wadau wa mradi wa “LNG” DAR

1

Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe akifungua warsha ya siku mbili kwa Wadau wa Mradi wa kusindika gesi asilia nchini (LNG) jijini Dar es Salaam.

 

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katikati ya juma liliandaa warsha ya siku mbili ya Wadau wa Mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika kwa ajilia ya kusafirisha nje ya nchi na matumizi ya nchini (LNG).

Akifungua Warsha hiyo kwa Niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe alisema warsha hiyo inalenga kuwakutanisha wadau wanaoshiriki katika utekelezaji wa Mradi huo.

“Warsha hii pia imekusudia kutengeneza mazingira shirikishi kwa wadau hao kabla ya kuanza kutekeleza ujenzi wa Mradi huo” alisema Prof. Mdoe.

Alisema msukumo mkubwa wa Taifa kwa sasa ni kuelekea kuwa nchi ya viwanda na kichocheo kikubwa cha kufikia lengo hili ni matumizi ya rasimali ya gesi kutumika kama nishati.

“Ni shauku yangu kwa sasa ni kuona Tanzania inavyojivunia fursa za uwekezaji hususani katika tasnia ya gesi asilia”, alisema Prof. Mdoe.

Hata hivyo alisema kufuatia kuwepo kwa gesi yakutosha kutasukuma utekelezaji mradi wa Mradi wa kusindika gesi asilia nchini.

Aliongeza kuwa ushirikishwaji wa wadau muhimu na elimu ndiyo makusudi makuu ya warsha hiyo kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mradi huo.

Aidha, akufunga warsha hiyo kwa niamba ya Mkurungezi Mtendaji wa TPDC, Mkurugenzi wa Usafishaji, Usafirishaji na Usambazaji wa Gesi Asilia, Dk. Wellington Hudson alisema warsha hiyo ilikuwa ya mafanikio makubwa kwa kuwakutanisha wadu muhimu wa Mradi wa kusindika gesi asilia nchini.

Alisema licha ya kutarajiwa kujengwa kwa Kiwanda cha kusindika gesi asilia nchini kwa kusafirisha gesi asilia nje ya nchi pia gesi asilia itatumika kwa soko la nchini na Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa mada zilizo wasilishwa katika katika warsha hiyo zilikuwa na tija kubwa katika kuelekea utekelezaji wa Mradi huo.

Ujenzi wa Kiwanda cha kusindika gesi asilia kwa matumizi ya ndani na kusafirisha nje ya nchi unatarajiwa kujengwa eneo la Likong’o katika Manispaa ya Lindi na unatarajia kugharimu Dola za Kimarekani bilioni 40 hadi 60.

Warsha hiyo imewakutanisha wadau kutoka Wizara ya Nishati na Madini, TPDC, Taasisi kutoka Serikalini na Makapuni ya Wawekezaji ya Mafuta na Gesi Nchini.