2

TPDC Yachangia Milioni 10 Kujenga Ofisi ya Mtaa

1

Kaimu Mkurugenzi Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapulya Musomba akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 10 Mwenyekiti wa Mtaa huo Bw. Geofrey Chacha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mji Mpya-Pugu Mjohe Jijini Dar es Salaam, katikati ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bi. Elizabeth Thomas.

2

Kaimu Mkurugenzi TPDC Mhandisi Kapulya Musomba akizungumza na wakazi wa Mtaa wa Mji Mpya-Pugu Mjohe kabla ya kukabidhi hundi ya Shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa huo.

3

Wakazi wa Mji Mpya – Pugu Majohe wakifurahia mara baada ya kukabidhiwa hundi ya shilingi milioni 10 kutoka TPDC kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania Nchini (TPDC) limeipatia shilingi milioni 10 Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mji Mpya iliyopo Pugu Majohe Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya mtaa huo.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano Jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Mhandisi Kapulya Musomba alisema wameamua kutoa fedha hizo kutokana na wakazi wa eneo hilo kuwa wadau muhimu wanao kupitiwa na bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

“TPDC hatuwezi kulinda bomba hili la gesi kila mahali linapopita, wadau hawa wamekuwa ni sehemu ya kulinda bomba hili wanalinda pia uchumi wa nchi kwa sababu gesi hii pia inatumika kuzalisha umeme zaidi ya asilia 50 nchini ” Alisema Musomba.

Aidha, Mhandisi  Musomba  ametoa wito kwa wananchi wa Pugu Majohe  kuacha kuchimba  mchanga  karibu  na  bomba hilo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaharibu miundombinu ya bomba hilo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bi.Elizabeth Thomas ameishukuru TPDC kwa kuwawezesha kupatikana kiasi hicho cha fedha kwani kitawasaidia katika ujenzi wa Ofisi hiyo na pia katika maendeleo ya Pugu Majohe na kuwaomba kuendelea kusaidia katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Ilala.

Nae, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mji Mpya-Majohe, Bw. Geofrey Chacha amesema kuwa ni faraja sana kupata msaada huo kutoka TPDC kwani utaweza kusaidia kumalizia ujenzi wa Ofisi yao.

Mchango huu umetupa nguvu katika kuwahamasisha wananchi katika eneo hili kuweza kuwa walinzi wazuri wa miundombinu hii ambayo inagusa maslahi ya Taifa letu” alisema Chacha.

TPDC kupitia Sera yake ya Uwajibikaji kwa Jamii imekuwa ikisadia sehemu ya mapato katika nyanja mbalimbali zikiwemo maji, afya, elimu, utawala bora na michezo.