3

TPDC Kuhakikisha ujenzi wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia unaleta tija kwa taifa.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi eneo la Madimba Mkoani Mtwara.

 

Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inatekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha na mitambo ya kusafisha gesi asilia kutoka Mtwara (Madimba) na Lindi (Songo Songo) hadi Dar es Salaam. Utekelezaji wa mradi huu ni hatua za makusudi za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kuongeza njia mbadala za kuzalisha nishati hiyo. Matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme hapa nchini yameanza miaka 10 iliyopita kwa kutumia gesi asilia ya Songo Songo (1974) na Mnazi Bay (1982).

Kati ya mwaka 2002/ 2004 ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha na kusafisha gesi asilia ilijengwa huko Songo Songo. Mradi huu ulihusisha bomba la kilometa 225 linalopita baharini na nchi kavu kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam pamoja na mitambo ya kusafisha kiasi cha futi za ujazo milioni 70 kwa siku za gesi asilia. Hata hivyo miundombinu hii ilifikia kikomo cha usafirishaji na usafishaji baada ya miaka minne tangu kuanza kutumika kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya gesi asilia hususan katika kuzalisha umeme.

Kutokana na kujaa kwa miundo mbinu hii, makampuni yanayojishughulisha na utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi hapa nchini yakiwemo Songas na Rakgas yalijitokeza kupendekeza jinsi aidha ya kupanua miundombinu iliyopo ama kujenga miundombinu mipya. Kwa mfano Songas walipendekeza upanuzi wa mitambo ya Songo Songo na kuweka mfumo wa ukandamizaji (Compression System) ambayo ingeongeza usafirishaji wa gesi kwa futi za ujazo milioni 35 kwa siku.  Rakgas walifanya uchambuzi yakinifu wa ujenzi wa miundombinu mipya ambao ungeunganisha usafirishaji wa gesi ya Mnazi Bay na Songo Songo.

Kwa kuzingatia umuhimu wa umiliki wa miundo mbinu hii pia kutokana na uzoefu uliopatikana kwa miundombinu iliyopo kumilikiwa na makampuni binafsi, Serikali iliona umuhimu wa kujenga na kumiliki miundombinu mipya ambayo inaweza kukidhi soko na mahitaji ya gesi asilia nchini. Maamuzi haya ya Serikali yalifuatiwa na zoezi la upembuzi yakinifu (Feasibily Study) mwaka 2010 ambapo ulifuatiwa na utafutaji wa fedha za kuwekeza katika kujenga miundombinu ambayo itakuwa ni mali ya Serikali kwa asilimia 100%.

Urafiki na Ushirikiano wa miaka mingi kati ya Tanzania na China ndio uliopelekea upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia. Katika kiasi hiki, asilimia 95% kutoka China huku Serikali ya Tanzania ikichangia asilimia 5%. Gharama za kulipia mkuza na kusimamia mradi zimelipwa na Serikali kupitia TPDC kwa asilimia 100%.

Mwaka 2011 TPDC ilitiliana saini ya makubaliano (Memorandum of Understanding) na Mkandarasi kutoka China, China PetroleumTechnology and Development Corporation (CPTDC) na mwaka huo huo mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya kusafisha na kusafirisha gesi asilia kati ya TPDC na CPTDC ulisainiwa.

3 thoughts on “TPDC Kuhakikisha ujenzi wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia unaleta tija kwa taifa.”

  1. I am working to invite you to participate in the exhibitions during the Local Government week in Mtwara where all Local Government representatives from all over the country will convey

  2. nina imani na TPDC katika ujenzi wa taifa letu. nimefurah sana mlipochangia ujenzi wa maabara kilwa, n.k. you the best company for gas production

Comments are closed.